Baadhi yetu, tunaoamini katika mabadiliko ya kweli tuko nyuma ya Rais Magufuli kwa sababu tunaamini anaongoza na siyo kutawala tu. Kama kiongozi, anaonesha njia, ameweka malengo na mwelekeo anautaka na anatuongoza kuelekea huko. Kama mtawala angeweza kabisa kuendelea na ilivyokuwa na mambo yale yale akikubali kusukwasukwa na mawimbi ya maoni na mawazo ya kila namna kutoka kila kona. Lakini yeye kama kiongozi anajua anataka kufanya nini.
Tayari tunajua msimamo wake kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma na madaraka. Tunajua maono yake kuhusu tatizo la msingi za la nchi yetu – na tunajua suluhisho lake kubwa ambalo alilipendekeza katika muda wote wa kampeni – “hapa kazi tu”.
Kuna wakati wa siasa na porojo na kuchangamsha genge. Chini ya Magufuli porojo, siasa na kuchangamsha genge havitakuwa na nafasi kubwa kwani sasa tunaelekea kuanza kujenga upya taifa letu, na inaonekana tunaanza kujenga kuanzia chini tena kwani tulifikiri tumefikia mahali pa kupaua na kugundua kuwa misingi yenyewe haikuwa sahihi au imebomolewa.
Tunasimama nyuma ya Rais kwa sababu tunatambua kuwa jambo kubwa kabisa ambalo analisimamia na limeelezwa vizuri na Makamu wa Rais – Bi. Samia Suluhu Hassan – jana ni kuwa kazi yao kubwa ni kuleta nidhamu. Na nidhamu inasumbua. Kuwataka watu wakae kwenye mstari wakati wamezoea kuchomoka chomoka ni kazi sana hasa kama kule kuchomoka chomoka kulikuwa kunawafanya waishi mjini. Tunaunga mkono nidhamu hii kuanzia ya matumizi ya fedha, matumizi ya muda, na matumizi ya raslimali zetu; nidhamu ya matumizi sahihi ya vipaji na vipawa vyetu, ujuzi wetu na uwezo wetu. Nidhamu hii kuirejesha na kuidumisha kunahitaji uongozi unaotambua kuwa – kama wanamuziki walivyoimba zamani – “nidhamu ya kazi ni msingi wa mafanikio mema kazini” ndio njia pekee ya kuweza kujenga jamii ya watu waliofanikiwa.
Tunatambua bila nidhamu ya kweli juhudi zote za kujiletea maendeleo zitakwama. Tunasimama nyuma ya Rais kwa sababu tunaamini kuwa kwa wakati huu na zama hizi mpya Tanzania inamhitaji kiongozi ambaye siyo tu anajua anachotaka kufanya lakini pia anaonesha namna ya kufanya yeye mwenyewe.
Tunatambua pia kuwa kiongozi baada ya kusikiliza maoni na mapendekezo mbalimbali mwisho wa siku ni lazima aamini katika uwezo wake, malengo yake na uthubutu wake wa kutenda na kusimamia kile anachotaka kufanya. Magufuli hadi hivi sasa anafanya kazi nzuri na yenye kustahili pongezi kwani kwa mara ya kwanza tunaweza kuona ni jinsi gani taifa lilikuwa limedeka na kudekezwa katika namna fulani ya maisha kiasi kwamba ikawa ni starehe. Starehe hii sasa imeisha na watu wanatakiwa kuamka na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na uongozi.
Kiongozi anatakiwa kuongoza na siyo kufuata; Magufuli sasa anaongoza. Tuko nyuma yake, tunamuunga mkono! Na binafsi naamini anaongoza kidemokrasia zaidi wakati huu kwani anatumia ipasavyo matokeo ya uamuzi wa kidemokrasia kufikia malengo yake ya kampeni. Go Magufuli Go!