JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO MAELEZO YA KAIMU MKURUGENZI MKUU, MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA, ENG. JAMES KILABA KUHUSU UAMUZI KUHUSU UKIUKWAJI WA MASHARTI YA USAJILI WA NAMBA/LAINI ZA SIMU ZA MKONONI
Ndugu Waandishi wa Habari,
Tumewaita hapa leo ili kutoa uamuzi kuhusu mashauri ya ukiukwaji wa masharti ya usajili wa namba/laini za simu za mkononi uliofanywa na makampuni ya simu za mkononi.
Makampuni hayo ni:
1. Airtel Tanzania Limited,
2. Benson Informatics Limited ambayo inatumia jina la biashara la SMART,
3. MIC Tanzania Limited ambayo inatumia jina la biashara la TIGO,
4. Viettel Tanzania Limited ambayo inatumia jina la biashara la Halotel,
5. Vodacom Tanzania Limited,
6. Zanzibar Telecom Limited ambayo inatumia jina la biashara la Zantel.
Makampuni hayo yamekiuka masharti ya usajili wa laini na matumizi ya laini kama yalivyoaninishwa kwenye Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 na Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za Leseni za 2011.
Kabla ya kuelezea uamuzi huo, naomba kwanza nitoe maelezo ya awali kuhusiana na suala zima la usajili wa laini/namba za simu za mkononi.
Itakumbukwa kwamba usajili wa namba simu umekuwa ni wa lazima baada ya sheria ya EPOCA ya 2010 kuanza kutumika. Kifungu cha 102(1) cha EPOCA kinafafanua kwamba mtu yeyote ambaye anamiliki simu ya mkononi ana jukumu la kutoa taarifa kwa mtoa huduma ikiwa kutakuwepo na mabadiliko ya umiliki wa simu hiyo au namba iliyosajiliwa kwa jina lake. Kifungu 102 (2) kinamtaka yeyote ambaye atataka kutumia simu au namba ambayo ilikuwa inatumiwa na mtu mwingine kusajili simu na namba hiyo. Aidha Kanuni za Watumiaji (The Electronic and Postal Communications (Consumer Protection) Regulations 2011) na Kanuni za leseni (Licensing Regulations 2011) zina vipengele kuhusu usajili wa namba za simu.
Kanuni ya 10(2) ya Kanuni za watumiaji kinasema mtu yeyote ambaye anamiliki au ana nia ya kutumia laini ya simu au kifaa chenye laini ya simu ndani anatakiwa kujisajili kwa mtoa huduma au wakala aliyeidhinishwa.
Kanuni ya 33(1) ya Kanuni za leseni kinaeleza kwamba mtu yeyote ambaye anauza au kwa namna yeyote ile anatoa laini ya simu au kifaa chenye laini ya simu ndani anatakiwa kuandikisha wateja kwa kutumia fomu maalum ambayo inamtaka mtumiaji atoe kitambulisho chenye picha yake halisi.
Sababu za kuanzisha utaratibu wa kusajili namba za simu ni pamoja na:-
(i) Kuwalinda watumiaji na jamii kutokana na matumizi mabaya ya huduma za mawasiliano.
(ii) Kuwezesha kuwatambua watumiaji wa huduma za ziada za simu, kama huduma za kibenki, kutuma na kupokea fedha, kufanya malipo mbalimbali kwa kutumia simu kwa mfano kulipia huduma za maji, umeme, vipindi vya televisheni vya kulipia n.k.
(iii) Kuimarisha usalama wa taifa.
(iiii) Kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano kuwafahamu vizuri wateja wao na kuwahudumia ipasavyo kadri ya mahitaji yao.
(v) Kuwa na taarifa za matumizi ya simu za mkononi kwa ajili ya mipango ya maendeleo ya sekta.
Mnamo Aprili 2013 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na makampuni yanayotoa huduma za simu za mkononi walikubaliana juu ya hatua za kumaliza kasoro zilizokuwa zimejitokeza katika usajili wa namba za simu. Aidha walikubaliana kutokuwezesha laini/namba za simu kutumika kabla ya usajili kukamilika na taarifa za mteja kuhakikiwa.
Makubaliano mengine yalikuwa kwamba mitandao ya simu isifanye kile kinachoitwa ‘ usajili wa awali’.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa usajili wa namba za simu.
Hivi karibuni, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekagua mifumo ya usajili wa laini za simu na kugundua ukiukwaji katika maeneo manne:
1. Namba kutolewa bila mteja kutakiwa kusajiliwa.
2. Namba kusajiliwa kwa majina, vitambulisho na nyaraka za watu wengine.
3. Namba kutokufungwa hadi usajili ukamilike
4. Namba kusajiliwa usajili wa awali.
Makampuni sita ambayo yaligunduliwa kutenda makosa hayo yote au baadhi yaliitwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania tarehe 2 na 3 Juni 2016 na kutakiwa kutoa utetezi wao kuhusu ukikwaji wa masharti ya Usajili wa namba za simu za mkononi.
Kufuatia kusikilizwa kwa mashauri hayo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilifikia uamuzi ufuatao kwa kila kampuni ya simu za mkononi husika:
UAMUZI:
Baada ya kusikiliza utetezi wa Mtoa Huduma kwa maelezo ya mdomo na maandishi, na baada ya kuzingatia utetezi huo, ni wazi kwamba Mtoa Huduma amekiuka kanuni ya 33 ya Kanuni za Leseni za mwaka 2011 zilizotolewa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) na pia amekiuka vifungu 93,130 na 131 vya Sheria hiyo.
Kwa kuzingatia kwamba ni wajibu wa Mtoa Huduma kuhakikisha kwamba uuzwaji na utoaji wa laimi za simu unafanyika kwa mujibu wa kifungu 93 (2,3 na 4) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya 2010, na Kanuni ya 33 ya Kanuni za Leseni za 2011 na kwamba Mtoa Huduma amekiuka matakwa ya Sheria; na
KWA KUTAMBUA KWAMBA matumizi mabaya ya laini/ namba za simu za mkononi kunahatarisha usalama wa Taifa na kunachochea tabia hatarishi katika jamii na kunaendeleza tabia za kiuhalifu nchini;
KWA HIYO BASI, Mamlaka inatoa AMRI kama ifuatavyo:
1. AIRTEL TANZANIA LIMITED ilipe kwa Mamlaka,ifikapo 30 Julai 2016 faini kama ilivyoainishwa hapa:
(a) SHILINGI 74,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Sabini na Nne) kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 148 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi.
(b) SHILINGI 33,500,000 (shilingi za Kitanzania Milioni thelathini na tatu na laki tano) kwa kuruhusu laini 67 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili.
(c) SHILINGI 32,500,000 (shilingi za Kitanzania Milioni thelathini na mbili na laki tano) kwa kuruhusu laini 65 ziwashwe kabla ya kuuzwa; na
(d) SHILINGI 42,500,000 (shilingi za Kitanzania Milioni arobaini na mbili na laki tano) kwa kuruhusu laini 85 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
2. BENSON INFORMATICS LIMITED ilipe kwa Mamlaka,ifikapo 30 Julai 2016 faini kama ilivyoainishwa hapa:
(a) SHILINGI 7,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Saba) kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 14 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi.
(b) SHILINGI 7,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Saba) kwa kuruhusu laini 14 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili; na
(c) SHILINGI 3,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Tatu) kwa kuruhusu laini 6 ziwashwe kabla ya kuuzwa.
3. MIC TANZANIA LIMITED ilipe kwa Mamlaka,ifikapo 30 Julai 2016 faini kama ilivyoainishwa hapa:
(a) SHILINGI 93,500,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Tisini na Tatu na Laki Tano) kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 187 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi;
(b) SHILINGI 43,500,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Arobainii na tatu na laki tano) kwa kuruhusu laini 87 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili;
(c) SHILINGI 41,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Arobaini na Moja) kwa kuruhusu laini 82 ziwashwe kabla ya kuuzwa; na
(d) SHILINGI 11,000,000 (shilingi za Milioni Kumi na Moja) kwa kuruhusu laini 22 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
4. VIETTEL TANZANIA LIMITED ilipe kwa Mamlaka,ifikapo 30 Julai 2016 faini kama ilivyoainishwa hapa:
(a) SHILINGI 36,500,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Thelathini na sita Laki Tano) kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 73 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi.
(b) SHILINGI 36,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Thelathini ba Sita) kwa kuruhusu laini 72 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili; na
(c) SHILINGI 34,500,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Thelathini na Nne Laki Tano) kwa kuruhusu laini 69 ziwashwe kabla ya kuuzwa.
5. VODACOM TANZANIA LIMITED ilipe kwa Mamlaka,ifikapo 30 Julai 2016 faini kama ilivyoainishwa hapa:
(a) SHILINGI 49,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Arobaini na Tisa) kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 98 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi;
(b) SHILINGI 24,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Ishirini na Nne) kwa kuruhusu laini 48 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili;
(c) SHILINGI 19,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Kumi na Tisa) kwa kuruhusu laini 38 ziwashwe kabla ya kuuzwa; na
(d) SHILINGI 4,500,000 (shilingi za Milioni Nne na Laki Tano) kwa kuruhusu laini 9 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
6. ZANZIBAR TELECOM LIMITED ilipe kwa Mamlaka,ifikapo 30 Julai 2016 faini kama ilivyoainishwa hapa:
(a) SHILINGI 36,500,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Thelathini na sita na Laki Tano) kwa kuruhusu kuuzwa kwa laini 73 bila kutumia kitambulisho halisi cha mnunuzi;
(b) SHILINGI 11,500,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Kumi na Moja na Laki Tano) kwa kuruhusu laini 23 ziuzwe bila kujaza fomu ya usajili;
(c) SHILINGI 7,000,000 (shilingi za Kitanzania Milioni Saba) kwa kuruhusu laini 14 ziwashwe kabla ya kuuzwa; na
(d) SHILINGI 2,000,000 (shilingi za Milioni Mbili) kwa kuruhusu laini 4 zifanyiwe usajili wa awali na kutumika kwenye mtandao wake.
Pamoja na faini hizi, Watoa huduma hawa wametakiwa kuchukua hatua zifuatazo:
a) Kuwasilisha Mamlaka a Mawasiliano Tanzania ifikapo 15 Julai 2016 orodha iliyohakikiwa ya wakala wa kusambaza na kuuza laini za simu nchi nzima kama inavyotakiwa na kifungu 92(2) cha EPOCA;
b) Kuacha mara moja kuwatumia wakala au wasambazaji wasioruhusiwa kuuza au kusambaza laini za simu nchini;
c) Kuhakikisha kwamba laini za simu zinauzwa na Wakala anayetambuliwa na Mtoa Huduma na ambaye ana anwani ya makazi inayofikika na pia mwenye Namba Tambulishi ya Mlipa Kodi (Tax Payer Identification Number); na
d) Kuzima laini zote zilizo sokoni ambazo zimewashwa na kuwasilisha taarifa ya utelekezaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ndani ya siku saba kutoka tarehe walizopokea Uamuzi huu.
Mtoa Huduma yoyote atakayekaidi utekelezaji wa AMRI atachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwa makosa ya jinai.
Mwisho, napenda kumalizia uwasilishaji wa uamuzi huu kwa kusisitiza yafuatayo:
Utaratibu wa kusajili laini za simu za mkononi unawahusu watoa huduma na watumiaji pia. Watumiaji, watoa huduma, wakala wa makampuni ya simu za mkononi na wananchi kwa ujumla wanakumbushwa kwamba ni kosa kisheria kutumia au kuwezesha kutumiwa kwa namba ya simu ambayo haikusajiliwa.
Ni kosa la jinai kutumia namba ya simu isiyosajiliwa. Adhabu ni faini ya shilingi laki Tano au kifungo cha miezi mitatu. Kusajili nenda kwa mtoa huduma wako au wakala wake ukiwa na kitambulisho chenye picha yako. Toa taarifa sahihi.
Aidha ni kosa kusajili laini kwa kutumia majina yasiyo sahihi.
Watumiaji wote ambao hawasajili namba zao za simu wafanye hivyo mara moja. Kuthibitisha usajili wako piga *106#.
Asanteni kwa kunisikiliza.
IMETOLEWA NA:
KAIMU MKURUGENZI MKUU,
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA