“Watanzania wanataka maisha ya kisasa lakini wengine hawataki kulipia gharama ya maisha hayo ya kisasa”

Neno la Leo: Watanzania wanataka maisha ya kisasa lakini wengine hawataki kulipia gharama ya maisha hayo ya kisasa. Wanataka wawe kama Marekani, Japan, China, Ulaya lakini wakiambiwa walipe hiyo gharama wanakuja juu! Sasa kwani Marekani, Japan, China, Ulaya zilishushwa toka Mbinguni zikimeremeta? Au wanafikiria haya mabarabara, mabasi na matreni yanayokimbia kama yanafukuzwa na radi yalikuja tu ghafla bin vuup! Kwamba, vyuo vyao vikuu vimeweza kufikia kutoa wataalamu wenye ubunifu wa kila namna kwa sababu Mungu anawapenda saaana hao na anatuchukia sisi?

Au watu wanafikiri – na nimeshawahi kukutana na watu wa aina yao – kwamba Mzungu kapendelewa saaana kwa sababu mweupe!? Au ni kweli tunaamini maneno tunayoambizana “Waafrika sisi tumelaaniwa” halafu tunaishi kama watu waliolaaniwa kutimiza unabii wetu wenyewe?

Nilisema juzi kuishi kwa njia ya mkato kuna raha yake hasa kama njia ya mkato haikufanyi utoke jasho! Hatuwezi kuwa na maisha ya kisasa na kujenga jamii ya kisasa yenye ubora wa maisha kwa kila namna bila kulipa gharama ya kufanya hivyo. Nje ya hapo tutaendelea kutamani tu samaki wa picha na mchuzi wa jirani!

MMM

Leave a Reply