Na Peter Sarungi (The Next Speaker)
Huu ni mwendelezo wa kuonesha jinsi gani imani zetu zinavyo changia kueneza fikra potofu kwa jamii juu ya watu wenye ulemavu.
Kumekuwa na tabia inayotokana na imani za baadhi ya mathehebu ya kikristu kutumia miujiza ya kuponya matatizo za watu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kukuza imani za waumini wao. Moja ya matatizo ambayo yamekuwa yakiaminishwa kwa waumini ni uwepo wa binadamu mwenye ulemavu. Baadhi ya Viongozi wa dini wamekuwa wakiaminisha waumini wao kwamba Ulemavu ni upungufu, kasoro na uumbaji usio kamilika. Wanaenda mbele zaidi na kuaminisha jamii kwamba Ulemavu ni Kazi ya shetani inayo stahili maombi na kumwomba Mungu afanye miujiza yake ya kubadilisha uumbaji huu wa shetani. Wanaamini kuwa mlemavu ni kufungwa na minyororo ya mateso ya shetani, wanaaminisha waumini sababu ya watu wenye ulemavu wengi kuwa masikini na wasioweza ni kutokana na ulemavu ulio letwa na shetani..
Je, ni kweli watu wenye ulemavu wana kasoro ya muumba?, je ni kweli uumbaji huu ni kazi ya shetani?, je ni kweli kuumbwa na ulemavu ni kufungwa na mateso ya shetani?
Bahati mbaya maombi yasipo zaa matunda yaliyo tarajiwa basi lawama zitatupwa kwa mlemavu kama mtu usiye na imani ama mwenye dhambi nyingi au utaambiwa wazazi wako au babu na bibi zako walitenda dhambi au waliingia maagano na shetani ndio maana unashindwa kupona. Hali hii inatufanya watu wenye ulemavu kujikataa wenyewe, kujiona wadhaifu mbele za Mungu, kusubiria miujiza kwa muda mrefu bila kuchukua hatua. Mnasababisha tunashindwa kuhudhuria mafundisho ya imani maana unahisi nikiingia kanisani basi mada ya mafundisho itabadilika na kuwa ulemavu wangu.
ADD Friends Campaign itafika hadi kwenye makanisa na misikiti ili kutoa elimu hii ili viongozi wa dini wasaidie kuelimisha jamii na kuondokana na fikra potofu juu ya ulemavu.
Ungana nami katika kujenga jamii yenye usawa wa imani na fikra juu ya ulemavu.