Miaka kadhaa nyuma, tulikuwa safarini kwenda Msumbiji, nakumbuka brother Zitto Kabwe pia tulikuwa naye kwenye msafara ule. Tulipanda ndege ya Shirika la ndege la Kenya kupitia Nairobi kisha Maputo.
Tukiwa njiani wakati wa kurudi nilipanda ndege nikiwa nafanya utani wenye kufanana na ukweli, “Hivi yaani sisi taifa kubwa tunashindwa na Kenya kumiliki ndege zetu kuja nchi jirani ya Msumbiji tu?”
Mhudumu wa ndege ile ya KQ alinijibu kwa kucheka “Ahh, Nyie Watanzania mko na maneno mengi, mnapiga siasa sana, hamwezi kuwa na ndege ka hizi”
Majibu haya yalifanya nijisikie aibu na kunyamaza, Licha ya ukweli kuwa Tanzania tulipoteza ndege nyingi baada ya kuvunjika kwa Shirikisho la Afrika Mashariki mwaka 1977. Lakini bado kama Taifa tusingepaswa kuwa katika hali ya kukosa hata ndege moja ya kuimiliki mpaka kufikia leo.
Kwa vyovyote vile, atakayejitokeza kupinga au kubeza juhudi hizi za dhati za Mh Rais JPM katika kufufua Shirika letu la ndege ambalo ndicho kiungo muhimu katika kukuza Utalii na kutangaza nchi yetu katika kuongeza mapato ya kigeni, lazima atakuwa ni adui wa taifa na adui wa taifa hapaswi kuwa sehemu ya taifa letu.
Najua tumeanza na ndege ndogo mbili, lakini kufika tatu lazima moja na mbili tuzivuke. Tujivunie hichi chetu na tuendelee kuamini tupo katika wakati mzuri zaidi kama taifa kufikia malengo ya kuwa taifa la watu wa kipato cha kati.
Shime, viongozi wa Shirika la ndege Tanzania na Watanzania wote, tuwe mabalozi wazuri wa ndege zetu na tuzitunze na kuzithamini ndege hizi. Ndege hizi ni Fahari ya nchi yetu, Na ni Fahari yetu sote.
Van.