Baba naomba nianze kwa salamu; shikamoo baba!…….Baba naomba nikwambie dhumuni la barua hii si kukuomba hela za matumizi kwani hilo si tatizo langu kwa sasa! Pesa zipo tena wewe wenyewe ndio umeziweka hivyo nipo vizuri baba!
Baba ninachotaka kukwambia leo hii nakuomba utege masikio yako kwa makini sana baba yangu kwani mwanao nimejawa na hofu nyini sana! Wewe ni baba yangu ninaye kupenda sana na siku zote nilitembea bara-barani na kulala usingizi mnono sana nikijua tupo katika mikono salama! Lakini, sasa hivi uwoga umenishika sana, siyo tu kwa watu ambao siwajui bali hata kwa hawa wakuu wa mikoa yetu ulio wachagua. Na mbaya zaidi imani yangu juu yako imeshuka kwa kiasi kikubwa sana kitu ambacho si kizuri kabisa kwani wewe ni baba yangu!
Baba, naomba unisaidie kuelewa, kwani unampango wa kung’ang’ania madarakani? Au unataka nchi yetu iwe kama Rwanda ile ya mauwaji? Au kama Uganda ya Mseven? Au unatamani Tanzania iwe kama Congo ya Kabila, na Burundi ya Nkurunzinza?! Au iwe nchi ya ukabila kama ile nchi ya Jomo Kenyatta?!! Mimi sijui baba lakini natamani kujua, tafadhali nijuze ili nijuwe kama nianze kuomba ukimbizi nchi za jirani?! Nakama ni hivyo je, zitakua ni nchi zipi katika bara hili la Africa?!!
Baba, niwapi mimi binti yako nikimbilie maana dalili zinaonyesha kama hali itaendelea kuwa hivi na wewe ukaendelea kubariki kwa mikono yako miwili basi mimi mwanao sina budi kuanza kukimbia kuomba hifadhi nchi za jirani hata ng’ambo ya Magharibi kama itaibidi! Japo natafakari sana je nitakimbia mwenyewe au nimchukuwe na mama? Vipi kuhusu bibi na babu? Bila kumsahau mjukuu wako kipenzi! ooh! vipi na yule dada yako wa pekee aliye olewa kijiji cha Koromije mkoani Mwanza? tena yeye ni mlemavu wa miguu! Na binamu yako Zainabu ambaye ni mlemavu wa ngozi huwa awezi tembea juani! Hawa wote nawapenda sana na itakuwa ngumu sana kwangu mimi kuishi mbali nao, nifanyeje baba? Hivi mida ipi itakuwa mizuri kwetu sisi kuanza mwendo; mchana au usiku? Baba, nguvu zinaniishia! Baba kwani niwapi tulikosea? Mbona mambo yanakuwa tofauti na ahadi zako? Mimi niliwashawishi ndugu zetu wote, majirani, marafiki, na Watanzania wote kwa ujumla kuwa wakupigie kura ya “ndio” kwani nina imani nawe, na kwa uchapa kazi wako ulionyesha kuwa wewe unafaa sana! Nao kwa furaha na nderemo wakakupitisha kwa kishindo kuwa Rais wa nchi yao. Nami mwanao nikatembea kifua mbele tena kwa mikogo na madaha mengi sana kuwa sasa Tanzania mpya inakuja! Tanzania ya amani tele, iliyo jaa demokrasia nyingi na uhuru wa kujieleza bila vitisho! Tanzania ya viwanda na miundo mbinu ya kisasa!
Baba, sasa mbona mambo yanakwenda sivyo?! Uliahidi kuleta uongozi bora ulio tukuka, uongozi wa haki na wakufuata sheria. Uliahidi kutulinda sisi wanawake na watoto, ukatuhakikishia kuidumisha amani ndani ya nchi yetu tuipendayo sana! Imekuaje sasa? mbona wavunja sheria ndio unawatukuza na kuwatunuku shahada za uongozi bora?! Baba ni wapi tumekukwaza? Mbona viongozi wanao tishia usalama wa maisha yetu kwa kuvamia sehemu zetu za kazi kwa mitutu ya bunduki ndio unao wapenda sana? Usalama wetu upo wapi? Mbona ndugu zangu hata hawaruhusiwi kuongea kwa uhuru bila kutolewa silaha za moto?!
Baba, nampenda sana kaka yangu ambaye ulimchagua kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es salaam. Nimchapa kazi sana hilo halina upinzani lakini baba yeye si mkamilifu, ana mapungufu yake kama mwanadamu yoyote yule; hivyo kubali kuwa sanyingine naye hukosea. Basi anastahili kuadhibiwa kama unavyo tuadhibu sisi wanao wengine kwa makosa tunayo yafanya au pale tunapo kukwaza!
Baba, sababu ya mimi na Watanzania wengine kuomba umuadhibu huyu kaka yetu, si mbaya hata kidogo! Hatuna nia ya kumkomoa au kumuumiza bali nikutaka kuweka mfano mzuri kwa wadogo zetu ambao wanakutizama iliwajifunze kitu fulani kuhusu utawala bora wa sheria na haki. Maamuzi yako yatatuaminisha kuwa unamaanisha kile usemacho. Kufanya hivyo kutaondoa hofu tulionayo Watanzania. Au unaogoapa hutopata mchapa kazi kama yeye? mbona kule kanda ya ziwa wapo wachapakazi wengi sana, tena watiifu, na waaminifu, hawana uonevu wala kiburi?!
Baba, naomba nimalizie kwa kusema samahani sana kama tumekukosea. Lakini ukumbuke tu kuwa wewe ni baba wa wengi na si wa mtu mmoja tu, hivyo tunaomba utupende, na utulinde wote bila ubaguzi wa aina yoyote! Usitugawe baba sisi sote ni wana wako. Sisi ni ndugu moja japo wengine ni wembamba na wengine wanene. Japo wengine wafupi na wengine warefu, wengine weusi wa rangi ya ngozi na wengi ni maji ya kunde; sisi ni ndugu moja. Usitubague wala kututenga!
Asante sana baba.