Category Archives: Jukwaa la walemavu

ADD Friends Campaign – Epsd 019: Adhabu ya Vyoo vya jamii kwa Watu wenye Ulemavu.

ADD Friends Campaign - Epsd 019:  Adhabu ya Vyoo vya jamii kwa Watu wenye Ulemavu.

Na Peter Sarungi (The Next Speaker)
Haja ndogo na kubwa ni moja ya matendo ya mwili ya lazima kwa viumbe vingi akiwemo binadamu. Umuhimu wake unatokana na kazi ya mfumo wa mkojo ambayo ni kutoa taka na sumu za mwili. Kwahivyo mwili huwa hauwezi kusubiri kwa mda mrefu badala yake kuna point inalazimika kutoa uchafu huo bila kujali uko katika mazingira gani.

Jamii inayo tuzunguka imekuwa ikitupa adhabu sana katika kupata huduma hii maana vyoo wanavyo jenga ni kwaajili ya kukidhi mahitaji yao ambayo mara nyingi kwa ustaarabu mdogo walio nao wengi wanachafua na kuweka hali hatarishi kwa jamii ya watu wenye ulemavu. Lakini pia vyoo hivyo vinakosa mazingira rafiki ya miundo mbinu kwa mtumiaji mwenye ulemavu kama vile vipimo vya milango, uwepo wa ngazi, maegemeo ndani ya choo, aina ya kifaa cha choo pamoja na uwepo wa maji safi na salama.

Jamii ya namna hii inayo tuzunguka haijali usalama wa afya na utu wa mtu mwenye ulemavu na hii ndio imekuwa ni changamoto kubwa kwa mtu mwenye ulemavu pale unapo amua kutoka katika mazingira uliyopo kwenda kwenye mazingira mageni wakati unapo toka ili kushiriki shughuli za uchumi, siasa na za kijamii.
Hili ni tatizo kubwa sana kwa mtu mwenye ulemavu, ni lazima awe mchaguzi sana katika kutafuta nyumba ya kupanga, awe makini sana katika kutumia vyombo vyetu vya usafiri wa umma, awe makini katika kuchagua mahala pa kufanya starehe na kadhalika.

#ADDfriends_Campaign tumeamua kubadili fikra hii ya mateso kwa mtu mwenye ulemavu. Ungana nasi kupaza sauti ili kujenga jamii ya walemavu iliyo salama.

Itaendelea.....

ADD Friends Campaign – Epsd 017 Tutakuwa Mubasha Azam Two Alhamisi asubuhi.

ADD Friends Campaign – Epsd 017
Tutakuwa Mubasha Azam Two Alhamisi asubuhi. 

Peter Sarungi (The Next Speaker)

Tunaendelea kutoa elimu mpya kwa jamii inayo zunguka watu wenye ulemavu ili kuondokana na fikra potofu.
Alhamisi 24/8/2017 Asubuhi ya saa mbili tutakuwa mubashara Azam Two tukijadili mada isemayo;

“Je nini kifanyike ili kuendeleza ustawi wa jamii ya watu wenye ulemavu nchini??”

Karibu tujadili na kujifunza wote. Kama una maoni, maswali na hata ushauri kuhusiana na mada hii una ruhusiwa kushiriki katika ukurasa wangu wa fb na tutazisoma hewani mubashara.

Karibu #ADDfriends tujenge ustawi mzuri kwa jamii ya walemavu.

ADD Friends Campaign – Epsd 013: Mchango wa Imani kueneza fikra potofu juu ya Ulemavu.~~~~Peter Sarungi

ADD Frriends Campaign - Epsd 013
Mchango wa Imani kueneza fikra potofu juu ya Ulemavu.
Peter Sarungi (The Next Speaker)
Habari marafiki zetu, leo ni moja kati ya siku za kuabudu kwa baadhi ya imani tulizo nazo nchini. Nami naomba nitumie siku hii kutoa ujumbe unao endana na siku hii lakini ukigusa kampeni yetu ya kuondoa fikra potofu juu ya watu wenye ulemavu.

Tabia, desturi na utamaduni ni moja ya vitu vinavyo tengeneza mitindo ya kuishi kwa jamii. Hata hivyo Imani ndio chanzo kikuu cha kutengeneza tabia, desturi, mila na utamaduni kwa jamii. Leo hii katika jamii zetu kuna mitindo mingi ya kuishi inayo akisi imani tulizo nazo. Imani ya mtu huonekana kupitia fikra zake, kwani kile mtu anacho kiamini ndicho atakacho kitenda.

Fikra potofu za jamii juu ya ulemavu ni moja ya zao linalo tokana na imani zetu katika jamii. Sipo kwaajili ya kupinga imani za watu lakini ni wajibu wangu kukataa imani kandamizi kwa walemavu. Imani zetu zimekuwa ziki tuaminisha kwamba moja ya makundi yenye kuhitaji misaada na huruma kutoka kwa jamii ni watu wenye ulemavu. Waumini wengi wamekuwa wakiamini kwamba ukimsaidia mlemavu basi unapata baraka na thwawabu kwa Mungu. Wanaamini walemavu wameumbwa ili kuwa chanzo chao cha baraka na mafanikio iwapo wata saidia kundi hilo.

Imani hii imejenga fikra ya kuwaona walemavu kama sehemu ya mtihani wa imani kwa jamii, imeleta fikra ya kuwaona walemavu kama viumbe walsio weza na hata ikitokea mlemavu huyo ameweza basi wataamini sio yeye wala jitihada zake bali ni Mungu. Yaani ni kama kobe unapo mkuta amepanda juu ya mti, lazima utasema kapandishwa.

Hizi ni fikra potofu zinazo tokana na mafundisho ya imani zetu. Kuna haja ya viongozi wa dini kubadilika haraka maana wakati ni huu ambao ADD Friends Campaign imefunguliwa maono yaliyo jificha kwa muda mrefu.
Ikiwa wewe unapata thwawabu kwa kunipa msaada wa siku moja, je mimi napata wapi hiyo thwawabu??? Au mimi si wa Mungu?? Au mimi naingia mbinguni bure??

Karibu ADD Friends tufikiri tofauti kwa pamoja ili kutibu jamii juu ya fikra potofu kwa watu wenye ulemavu.

ADD Friends Campaign – Epsd 014: Je, Ni sahihi kumwombea mlemavu apone Ulemavu? -Peter Sarungi

ADD Friends Campaign - Epsd 014
 Je, Ni sahihi kumwombea mlemavu apone Ulemavu?

Peter Sarungi (The Next Speaker)
Na Peter Sarungi (The Next Speaker)

Huu ni mwendelezo wa kuonesha jinsi gani imani zetu zinavyo changia kueneza fikra potofu kwa jamii juu ya watu wenye ulemavu.

Kumekuwa na tabia inayotokana na imani za baadhi ya mathehebu ya kikristu kutumia miujiza ya kuponya matatizo za watu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kukuza imani za waumini wao. Moja ya matatizo ambayo yamekuwa yakiaminishwa kwa waumini ni uwepo wa binadamu mwenye ulemavu. Baadhi ya Viongozi wa dini wamekuwa wakiaminisha waumini wao kwamba Ulemavu ni upungufu, kasoro na uumbaji usio kamilika. Wanaenda mbele zaidi na kuaminisha jamii kwamba Ulemavu ni Kazi ya shetani inayo stahili maombi na kumwomba Mungu afanye miujiza yake ya kubadilisha uumbaji huu wa shetani. Wanaamini kuwa mlemavu ni kufungwa na minyororo ya mateso ya shetani, wanaaminisha waumini sababu ya watu wenye ulemavu wengi kuwa masikini na wasioweza ni kutokana na ulemavu ulio letwa na shetani..

Je, ni kweli watu wenye ulemavu wana kasoro ya muumba?, je ni kweli uumbaji huu ni kazi ya shetani?, je ni kweli kuumbwa na ulemavu ni kufungwa na mateso ya shetani?

Bahati mbaya maombi yasipo zaa matunda yaliyo tarajiwa basi lawama zitatupwa kwa mlemavu kama mtu usiye na imani ama mwenye dhambi nyingi au utaambiwa wazazi wako au babu na bibi zako walitenda dhambi au waliingia maagano na shetani ndio maana unashindwa kupona. Hali hii inatufanya watu wenye ulemavu kujikataa wenyewe, kujiona wadhaifu mbele za Mungu, kusubiria miujiza kwa muda mrefu bila kuchukua hatua. Mnasababisha tunashindwa kuhudhuria mafundisho ya imani maana unahisi nikiingia kanisani basi mada ya mafundisho itabadilika na kuwa ulemavu wangu.

ADD Friends Campaign itafika hadi kwenye makanisa na misikiti ili kutoa elimu hii ili viongozi wa dini wasaidie kuelimisha jamii na kuondokana na fikra potofu juu ya ulemavu.

Ungana nami katika kujenga jamii yenye usawa wa imani na fikra juu ya ulemavu.

PIGO KWA JAMII YA WALEMAVU! R.I.P Mh. Dr Macha

Jamii ya watu wenye ulemavu imesikitika sana kupokea taarifa za msiba wa mama yetu na mtetezi wetu aliyekuwa anatuwakilisha bungeni kama mbunge viti maalum wanawake kwa upande wa walemavu Mh. Dr. Elly Macha kupitia Chadema Tanzania. Dr. Macha amefariki dunia akiwa nchini Uingereza kwenye Matibabu.

Binafsi mara ya mwisho kuonana na huyu mtetezi ni mwaka 2015 nilipokuwa naomba fursa ya kuwa spika, maneno yake yalinipa nguvu na sababu za kuendelea kutetea jamii ya walemavu katika nchi na hata kimataifa. Aliamini mabadiliko ya kuikomboa jamii ya walemavu yatapatikana kupitia walemavu wenyewe na ikiwa watashiriki katika vyombo vya maamuzi kama bunge, mahakama na hata ndani ya serikali. Bado naamini katika maneno yake na yataendelea kuishi na ipo siku yatatimizwa na walemavu wenyewe. 

Peter Sarungi (The next time)

Natoa pole kwa familia yake,jamii ya watu wenye ulemavu, ndugu, jamaa, marafiki, viongozi na wapenzi wote wa CHADEMA kwa kumpoteza mama yetu tuliye mpenda lakini Mungu amempenda zaidi yetu. Tuwe wavumilivu na wenye matumaini katika kipindi hiki kigumu huku tukiamini ipo siku tuta onana naye.

Amen  Nami naomba nitoe salamu zangu za pole nyingi sana kwa wana familia, ndugu, jamaa, marafiki, pamoja na jukwaa zima la walemavu Tanzania na duniani kote! Taifa limepoteza msomi mmoja ambaye pengo lake halito zibika!

Bwana ametoa na Bwana ametwaa jina lake libarikiwe!……. R.I.P Mh. Dr. Macha

MALENGO YA JUKWAA LA WALEMAVU TANZANIA. -na Peter Sarungi

 Nitumie fursa hii kutoa tafsiri ya katiba juu ya Malengo yake kwa kufuata Ibara ya II.C. Malengo hayo yatajumuisha yafuatayo.

  1.  Jukwaa litasimama kama sauti ya kuwakilisha maoni na mapendekezo ya watu wenye ulemavu.
  2. Kusimamia maoni na mapendekezo yanafanyiwa kazi katika vyombo vya serikali, mashirika, almashauri na taasidi mbalimbali wakati wa kuunda sera na sheria katika jamii.
  3. Kuratibu vikao, mikutano na makongamano ya kueneza na kukuza uelewa wa watu wenye ulemavu juu ya sera, taratibu na sheria katika kupata fursa mbalimbali za nchi.
  4.  Kujenga mahusiano na muingiliano mzuri kati ya jamii ya watu wenye ulemavu wenyewe na jamii zingine tukilenga ushirikishwaji katika kutumia fursa mbalimbali.
  5. Kufanya tafiti mbalimbali za maswala ya watu wenye ulemavu kwa kutumia chombo kitakachoundwa ili kutambua changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa sheria na sera mbalimbali zinazohusu watu wenye ulemavu.
  6. Kutoa taarifa mbalimbali zenye lengo la kubainisha fursa za kijamii, siasa na uchumi zilizopo kitaifa na kimataifa ili kuhamasisha ushiriki wa watu wenye ulemavu.
  7. Kuratibu uanzishwaji wa vikundi mbalimali vyenye malengo ya kuungana ili kupata fursa za uchumi na jamii ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa majukwaa madogo ya ukanda, mikoa,miji na vijiji katika kueneza sauti ya watu wenye ulemavu.
  8. Kushawishi, kutetea na kukuza haki na wajibu wa watu wenye ulemavu kupitia usimamizi wa sera na sheria No.9 ya watu wenye ulemavu.

Hayo ndio malengo hasa ya kuanzisha Jukwaa hili. Nitaanza kuchambua umuhimu wa kila lengo ili kujua uhitaji wa lengo hilo katika jamii ya watu wenye ulemavu.  

Tafadhali share, like, tag na comment kushiriki katika malengo haya ili jamii na wadau woye wapate taarifa.

Asanteni sana.

JUKWAA LA WATU WENYE ULEMAVU TANZANIA-na Peter Sarungi

Na Peter Sarungi (The next Speaker)

 Nitumie fursa hii kutoa shukurani kwa wote walio jitolea na hata kufuatilia kwa karibu juu ya uundwaji wa Jukwaa la Watu wenye Ulemavu Tanzania. Mpaka sasa tumekamilisha 95% ya taratibu za kusajili Taasisi hii muhimu kwa walemavu. Jamii ya watu wenye ulemavu imeendelea kutengwa katika mipango mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa sababu ya kukaa kimya bila kusema juu ya changamoto zetu, uwezo wetu, vikwazo tunavyokumbana navyo na hata mafanikio yetu. Ni muda sasa umefika wa kusema kwa nia ya kutetea na kushawishi maswala ya watu wenye ulemavu Tanzania ili na sisi Tanzania tufanane na wenzetu wa Afrika Mashariki walio amua kutekeleza kwa maneno na vitendo mkataba wa UN unao husu jamii ya walemavu na ni mkataba ambao Mh. Mkapa aliridhia na kusaini kisha Mh. Kikwete kuruhusu utungwaji wa sera na sheria no.9 ya watu wenye ulemavu na sasa kilichobaki ni kupiga kelele juu ya utekelezaji wake.

Ni jukumu letu sote kupiga kelele tena bila utengano na kwa sauti moja hata kama wewe sio mtu mwenye ulemavu lakini ukiguswa na hili basi ni sahihi kusema kwa nguvu hadi jamii, serikali na wadau wengine wapate kusikia ujumbe huu. Kuna msemo unasema hivi…

“Mtoto anayelia na kupiga kelele sana ndiye anaye pewa nyonyo na mama yake, ukinyamaza maana yake umeshiba”

Sidhani kama sisi watu wenye ulemavu tumeshiba katika nchi yetu, la hasha ila tuna ugulia kimya huku tukifa na tai shigoni. Ukimya wetu ndio unao tufunga, unao turudisha nyuma, unao tififisha ndoto zetu, unao tukosesha thamani na ndio sababu ya kutengwa na fursa.

Tanzania amka useme jambo kwa jamii hii ili na wewe ushiriki katika kutetea na kushawishi maswala ya watu wenye ulemavu Tanzania.