Najua mimi na wewe tunafamiana toka tukiwa wadogo lakini kwa faida ya wasomaji naomba ujitambulishe majina yako halisi: Asante, mimi ninaitwa Mahmoud Ramadhan Zubeiry, mtaani walizoea kuniita Mudi
Unaweza ukatuelezea kidogo kuhusu elimu yako? Shule ya msingi nilisoma pale Mgulani, baadaye nikaenada Rutabio sekondari kabla ya kufanya kozi mbili za awali za Uandishi wa Habari MAMET (Maarifa Media Trust), chuo ambacho kilikuwa kinamilikiwa na akina Jenerali Ulimwengu. Baada ya hapo, mwaka 2008 nilipata Stashahada ya Uandishi wa Habari ya LSJ (London School of Journalism) ambayo nilifanya online
Ilikuwaje mpaka ukaanzisha blog yako na kwanini uliiita binzubeiry?
Baada ya kufanya kazi za kuajiriwa kwa muda mrefu tangu mwaka 1999, katika magazeti ya Dimba, Mtanzania, Rai, Bingwa, The African na baadaye Tanzania Daima na Sayari hapa nyumbani nikaona sasa inatosha. Lazima nisimame kama mimi kutafuta mafanikio binafsi. Ndipo nikaamua kuanzisha blog, ambayo sasa imekuwa tovuti kamili ya michezo, www.binzubeiry.co.tz
Yalikuwa maamuzi magumu, ambayo mpinzani wa kwanza alikuwa mke wangu, pale nilipomuambia ghafla ninaacha kazi mwaka Mei mwaka 2012. Kama unavyojua mishahara ya kwenye vyombo vya habari hapa nyumbani haitoshelezi kukidhi mahitaji- hivyo niliacha kazi sina chochote. Sikuwa hata na kiwanja. Nilianza blog katika mazingira magumu sana, sina vifaa, nahangaika kusaka habari mitaani. Nilijituma hivyo hivyo hadi blog ikaanza kuvuma hatimaye nikaanza kupata watangazaji, taratibu nikaanza kununua vifaa vya kazi. Alhamdulillah sasa nina vifaa ambavyo ninafurahia kufanyia kazi, kuanzia kamera, MacBook na zagazaga zote. Nipo full, ila tu ofisi bado popote.
Hali ikoje leo?
Alhamdulillah ninamshukuru Mungu, watoto wangu wane kati ya watano wote wanasoma shule za kulipia, wawili kati wao sekondari kidato cha kwanza (Nurat na Precious). Wawili wapo shule ya msingi darasa la kwanza (Prince Akbar) darasa la pili (Princess Asia). Mungu akijaalia mwakani Sheikh Yussuf (miaka miwili) ataanza chekechekea. Nina shamba la embe ekari mbili eneo la Kigamboni. Nina nyumba Kigamboni huko huko na kiwanja ambacho hakijajengwa bado cha ukubwa wa 40-40.
Unamagari mangapi?
Yapo matatu tu, Passo anayotumia mke wangu, Range Rover na BMW ambazo natumia mwenyewe
Inaelekea unapenda sana michezo, je ulisomea uwandishi wa habari upande wa michezo au ni kipaji tuu ulizaliwa nacho?
Kama utakumbuka napenda michezo tangu nipo mdogo, nimecheza mpira mwenyewe pale KJ, lakini sikubahatika kufika mbali. Wakati nipo shule ya msingi Mgulani nilichaguliwa na Mwalimu Chale kama unamkumbuka katika kikundi cha Chipukizi, ambao ndiyo tulikuwa Ball Boys wa Uwanja wa Taifa enzi hizo mpira wa Tanzania uko juu sana. Kwa hivyo tangu hapo nikawa mpenzi sana wa michezo. Kwa kupenda kusoma magazeti, nikapenda sana na mimi siku moja niandike. Nilikuwa navutiwa wana na uandikaji wa watu kama Johnson Mbwambo na Francis Chirwa. Nilitamani siku moja niwe kama wao. Nashukuru walikuwa mabosi wangu, walinifundisha kazi katika gazeti la Dimba kwa upendo kabisa. Kama ninasifiwa leo ni Mwandishi mzuri wa michezo, basi kwa sababu nilipitia kwa walimu wazuri hao na wengine wengi kweli. Eric Anthony alikuwa Mhariri wangu wa kwanza pale Dimba. Huyu jamaa alinipiga msasa sana.
Ulipata wapi ujasiri wa kuanzisha blog yako mwenyewe?haswa ukitazama hapo nyuma watanzania walio wengi walikuwa wanafikiri kuanzisha blog ni lazima uwe mtu maharufu au mtu ambaye umetoka kwa familia yenye pesa?
Kama nilivyokuambia, niliamua tu kujilipua kwa kuacha kazi na kwenda kujiajiri mwenyewe. Nilijikabidhi kwa Mungu na leo ninamhsukuru sana Mungu kwa kweli. Amenisamamia na anaendelea kunisimamia. BIN ZUBEIRY ndiyo habari mjini
Hii blog unaitumia kama sehemu tuu ya vitu unavyo vipenda au pia ni sehemu ya kujiingizia kipato? Mama hii ofisi, inafanya niishi kupitia malipo ninayopata kutokana na vijitangazo hivyo. Ukiondoa hii tovuti, mimi mkulima na nina mpango kuanza mradi wa ufugaji nitakapohamia kwenye nyuma yangu Januari Mungu akipenda.
Najua watu wengi hawajui historia ya ulipo tokea ila kwa sisi tulio kufahamu tunaona ni ukuu wa miujiza ya Mungu. Je wewe ulisha wahi kuwaza wakati wa utoto wako kuwa ipo siku moja utaishi maisha haya unayo ishi sasa hivi? Labda udokeze kidogo maisha ulio kulia: Kuna wakati huwa nalia mwenyewe ninapokumbuka nilipotoka, misukosuko na shida za maisha nilizopitia. Lakini mwisho wa siku ninamshukuru Mungu tu, kwani yeye ndiye mpangaji wa yote. Niseme nini Alpha, mimi nimetokea familia ya kimasikini pale Keko wewe mwenyewe unajua. Tulikuwa na maisha duni kupita duni zote. Kuna wakati nilikuwa nakwenda kwenye jalala la soko dogo pale Keko kuokota vilivyotupwa na kutafuta vyenye nafuu ili twende nyumbani kupika kupata chakula. Nilianza kufanya deiwaka hata kabla sijaanza darasa la kwanza, napimisha watu uzito kwa mzani si unakumbuka? Na ni ule mzani ulinosomesha mimi, ilikuwa kila nikitoka shule naenda kusanya, Napata fedha za mahitaji ya shule. Nilikuwa nakwenda kubeba mizigo Kitumbini. Nimepiga debe, nimeuza mitumba minadani. Manyanyaso, chuki na masimango hivyo ni vya kawaida.
Wewe ni mtu au mwandishi wa habari pekee ulie bahatika kuona gari la kifahari (ambalo ni custom made) la kijana wa Bhakresa; ulijisikiaje ulipo pata fursa hiyo? Kwanza mlifahamiana wapi au ulimjuaje?
Yussuf ni rafiki yangu. Tumejuana kutokana na kazi, wao wanamiliki timu ile ya Azam FC. Alipenda ninavyoandika habari za timu yao, akawa rafiki yangu, tumeshibana hadi tumeaminiana kiasi hicho.
Na Yussuf pamoja na Zacharia Hans Poppe ni watu wenye mchango mkubwa katika maisha yangu. Hawa ni wafadhili wakuu wawww.binzubeiry.co.tz
Ni nini umejifunza zaidi au faida kubwa umepata kutokana na mitandao? Je unafikiri watanzania wanatumia vizuri mitandao?
Nimejifunza mengi sana, nilisahau kukuambia, nilisoma kozi moja fupi pia ya namna ya kuendesha blog mwaka 2012 ilidhaminiwa na SBL (Serengeti Breweries). Kuhusu matumizi, si Watanzania, watu dunia nzima wapo wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii. Na vigumu kuwabadilisha. Hizo ni hulka. Mtu anayejishimu hawezi kuposti picha za ngono. Hawezi kutumia mtandao kumtukana mtu.
Nini ujumbe wako kwa Watanzania wenzako?
Ujumbe wangu kwa Watanzania na vijana wenzangu. Wamtegemee Mungu, waache ushirikina. Mafanikio yanakuja baada ya kujituma. Lazima tufanye kazi, tuache majungu. Tanzania itaendelea zaidi, iwapo vijana watafanya kazi kwa bidii.