Wapendwa wasomaji wangu haswa wanawake wenzangu, naomba msinishangae kwanini sijazungumzia vifo vya kinyama vya wanawake wawili vilivyotokea wiki iliyopita. Kwanza nawapa pole wafiwa wote na familia zao, Mungu awape faraja katika mapito haya.
Pili, mimi maswala haya ya domestic abuse haswa kwa wanawake nilishawahi waeleze huko nyuma kuwa ni mambo ambayo sina nguvu sana ya kuyaelezea kwani vinakuwa vinanikumbusha maumivu makali sana ambayo sitaki kuyafikiria wala kuyazungumzia kwa sasa. Siku nikijiona nina nguvu ya kuongelea basi nitawaelezea. Ila kwa sasa acha watu kama akina Joyce Kiria wayaongelee. Ndio maana hata yule dada aliyeuliwa na mumewe kule London sikusema kitu siyo kwamba sijali ila ninakuwa na maumivu yaliyo changanyika na hasira hivyo naona ni bora kunyamaza kuliko kuongea nikiwa na hasira.
Tatu, wanawake wenzangu, hawa wanaouliwa haikutokea tu pasipo kuonyesha dadalili za ukatili ambazo zitaashiria kifo! Haya mambo yanaanza kidogo kidogo na kadri unavyojaribu kuvumilia ukatili huo unao uona ni mdogo ndio unavyomjengea mazingira mazuri ya kukumaliza kabisa! Kataa ukatili wa aina yoyote ile, Hawaanzi kwa kupiga huwa wanaanza kwa kukutenganisha na ndugu na marafiki zako wa karibu ili usiwe na msaada wowote. Ukisha ona mumeo au mpenzi wako anaonyesha dalili za kutaka utengane na ndugu zako au wazazi wako basi anza kulala macho wazi!! Halafu utakuta yeye ndio anataka wewe uonekane mbaya yupo busy kuongelea udhaifu wako kwa watu bila kusema makosa yake ogopa sana! Kwanza mwanaume anayekupenda hata mgombane vipi hawezi zungumzia matatizo yenu kwa watu, mtagombana wenyewe na kuyamaliza wenyewe!!
Ogopa sana mwanaume asiyejali hisia zako! Emotional abuse ni dalili kubwa ya pili katika maswala ya unyanyasaji. Akisha kutenga na ndugu zako basi lazima kinacho fuata ni ukatili wa kihisia na baada ya hapo atakupiga kama hata kuuwa basi atakuachia kilema cha maisha!
Jamani hii ni karne 21 nani bado anataka kuishi maisha ya zama za giza? Eti mwanaume anakupiga mpaka mimba inatoka halafu bado unamwita mume wangu? Au mtu eti mwanaume anakwambia utoe mimba kwasababu hataki watoto wa kike nawe unakubali??? halafu unjiita msomi?! ??
Jamani, Joyce Kiria anongea kwa sauti mwenye masikio na asikie asiyetaka shauri yake. Dalili huwa zinaanza mapema uwamuzi ni wako kuzikemea au kuzilea mpaka utolewe roho. Nachoomba tu tuwafundishe watoto zetu wa kike kwamba ukatili HAPANA! Napia watoto wetu wa kiume wafundishwe kupenda na kuheshimu wanawake kwani hata mama zao ni wanawake vile vile!