*Kesha la Asubuhi*
*Juma Nne*
*Kusafiri Pamoja na Wamisionari* ??Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao. Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro. Matendo ya Mitume 13:2-4.
??Ni jinsi gani tunauhitaji uwapo wa Mungu! Kwa ajili ya ubatizo wa Roho Mtakatifu, kila mtendakazi anapaswa kuwa anapumua maombi yake kwenda kwa Mungu. Makundi mbalimbali yanapaswa kukutana pamoja ili kumwita Mungu kwa ajili ya msaada maalum, kwa ajili ya hekima kutoka mbinguni, ili kwamba watu wa Mungu waweze kufahamu jinsi ya kupanga na kubuni jinsi ya kutekeleza kazi hiyo. Kwa namna ya pekee watu wanapaswa kuomba kwamba Bwana awachague mawakala wake, na kuwabatiza wamisionari kwa Roho Mtakatifu. Kwa siku kumi wanafunzi waliomba kabla baraka ya Pentekoste kuja. Ilihitajika muda kiasi kile kuwafikisha katika ufahamu wa kile kinachomaanishwa na kutoa maombi yenye kuleta matokeo yanayotarajiwa, kusogea karibu zaidi na zaidi kwa Mungu, kukiri dhambi zao, kunyenyekesha mioyo yao mbele za Mungu, na kwa imani kumtazama Yesu, na kubadilishwa kufanana na sura yake. Baraka ile ilipokuja, ilijaza mahali pote walipokuwa wamekusanyika; na huku wakiwa wamejazwa uwezo, waliondoka kwenda kufanya kazi yenye kuleta matokeo yanayotarajiwa kwa ajili ya Bwana.
??Inatupasa kuomba kwa bidii kwa ajili ya kushuka kwa Roho Mtakatifu kama vile wanafunzi walivyoomba katika siku ile ya Pentekoste. Iwapo walimhitaji [Roho yule] wakati ule, tunamhitaji zaidi leo. Giza la kimaadili, kama vile kitambaa cha maziko, linaifunika dunia. Kila aina ya mafundisho ya uongo, uasi, na madanganyo ya kishetani yanaongoza vibaya akili za wanadamu. Pasipo Roho na uwezo wa Mungu, itakuwa ni kazi bure kusumbuka kufanya kazi katika kuwasilisha ukweli. Ni lazima tuwe na Roho Mtakatifu ili apate kutuhimili katika mapambano haya; “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” (Waefeso 6:12).
??Hatuwezi kuanguka maadam tunamtumainia na kumwamini Mungu. Hebu kila roho ya kwetu, wachungaji na washiriki, iseme, kama Paulo alivyosema, “Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa” (1 Wakorintho 9:26), bali kwa imani na tumaini takatifu, katika kutarajia kupata thawabu. - Home Missionary, Nov. 1, 1893.
Related