*KESHA LA ASUBUHI*
_JUMATATU APRILI 23, 2018_
*Kutotumainia Maono Yetu* _Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako. Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako. Zaburi 119:15, 16._
✍? Mungu amewapa watu ujuzi ulio muhimu kwa ajili ya wokovu kwenye Neno lake. Maandiko Matakatifu yapasa yakubaliwe kama udhihirisho wa mapenzi yake wenye mamlaka, usiokosea. Maandiko Matakatifu ni kiwango cha kupimia tabia, mdhihirishaji wa mafundisho, na kipimo cha uzoefu. “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema” (2 Timotheo 3:16, 17).
✍? Hata hivyo, ukweli kwamba Mungu amedhihirisha mapenzi yake kwa watu kupitia kwa Neno lake hakujaondoa umuhimu wa kuwepo kwa Roho Mtakatifu na uongozi wake. Kinyume chake, ahadi ya Roho ilitolewa na Mwokozi wetu, ili afungue Neno kwa watumishi wake, aangaze na kuweka mafundisho yake katika matumizi. Na kwa sababu ni Roho wa Mungu aliyevuvia Biblia, haiwezekani kwamba mafundisho ya Roho wakati wowote yawe kinyume na yale ya Neno.
✍? Roho hakuletwa – wala kamwe hawezi kutolewa – ili kuizidi Biblia; kwani Maandiko yanasema wazi kabisa kwamba Neno la Mungu ni kipimo ambacho kwa hicho mafundisho yote na uzoefu ni lazima yajaribiwe. Mtume Yohana anasema, “Msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani” (1 Yohana 4:1). Naye Isaya anatamka, “Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi” (Isaya 8:20).
✍? Kazi ya Roho Mtakatifu imetupiwa lawama kubwa kutokana na maovu ya kundi la watu ambao, huku wakidai kuwa na ujuzi juu yake, wanadai kutokuwa na hitaji zaidi la uongozi kutoka kwenye Neno la Mungu. Hawa wanaongozwa na fikra ambazo wanadai kuwa ni sauti ya Mungu moyoni. Lakini roho anayewatawala siyo Roho wa Mungu. Hali hii ya kufuatilia fikra hizi, huku Maandiko yakipuuziwa, inaweza tu kufikisha katika machafuko, udanganyifu na uharibifu. Hii inaendeleza tu mipango ya yule mwovu.
✍? Kwa sababu huduma ya Roho Mtakatifu ina umuhimu mkubwa kwa kanisa la Kristo, ni mbinu ya Shetani, kupitia kwa makosa ya wenye itikadi kali na misimamo mikali, kutweza kazi ya Roho na kusababisha watu wa Mungu kupuuzia chanzo hiki cha uwezo ambacho Bwana wetu mwenyewe ametupatia. – The Great Controversy, uk. vii, viii.
*MUNGU AWABARIKI MNAPOTAFAKARI NENO*
Related