Kesha la asubuhi: UTAKATIFU

*Kesha la Asubuhi*

*J, tano Tarehe 28/3/2018*

*UTAKATIFU*

?? *Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao. Waebrania* *12:14*

??Tangu milele, Mungu alichagua watu wawe watakatifu. “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu” (1 Wathesalonike 4:3). Mwangwi wa sauti yake unatujia, daima ukisema, “Utakatifu zaidi, Utakatifu zaidi.” Na jibu letu daima yafaa liwe, “Ndiyo Bwana, watakatifu.”

??Hakuna mtu anayepokea utakatifu kama haki ya kuzaliwa, au kama zawadi kutoka mwanadamu mwingine yeyote. Utakatifu ni zawadi ya Mungu kupitia kwa Kristo. Wale wanaompokea Mwokozi wanakuwa wana wa Mungu. Hawa ndio watoto wake wa kiroho, waliozaliwa upya, waliofanywa upya katika haki na utakatifu wa kweli. Nia zao zimebadilishwa. Wanaona mambo halisi ya milele kwa maono yaliyo wazi zaidi. Hawa wamefanywa kuwa sehemu ya familia ya Mungu nao wanapatanishwa na sura yake, wanabadilishwa na Roho wake kutoka utukufu hadi utukufu. Kutoka katika kufurahia hali ya kupenda nafsi katika viwango vya juu sana, wanafikia hatua ya kufurahia upendo wa juu kwa Mungu na kwa Kristo. “Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo” (Warumi 5:1). Kuhesabiwa haki kunamaanisha msamaha. Kunamaanisha kwamba moyo, ukiwa umesafishwa na kuondolewa matendo yaletayo mauti, umeandaliwa kupokea baraka ya utakaso. Mungu ametuambia kile ambacho ni lazima tufanye ili tupokee baraka hii. “Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano, mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu” (Wafilipi 2:12-15).

??Upendo wa Mungu, ukihifadhiwa moyoni na kudhihirishwa katika maneno na matendo, utafanya sehemu kubwa ya kujenga na kuadilisha wanadamu kuliko jambo lingine lolote lile. Katika maisha ya Kristo, upendo huu uliweza kuonekana kikamilifu na bila upungufu. Msalabani pa Kristo, Mwokozi alifanya upatanisho kwa ajili ya jamii ya watu iliyokuwa imeanguka dhambini. Utakatifu ni tunda la kafara hii. Ni kwa sababu alikufa kwa ajili yetu ndiyo maana tunaahidiwa karama hii kuu. Hivyo ni shauku ya Kristo kutupatia karama hii. Ni shauku yake kwamba tuweze kuwa washirika wa tabia yake. Ni shauku yake kuokoa wale ambao kutokana na dhambi wamejitenga na Mungu. Yeye anawaita wachague huduma yake, wajitoe wenyewe kikamilifu kuwa chini ya utawala wake, wajifunze kutoka kwake namna ya kufanya mapenzi ya Mungu. – Signs of the Times, Des. 17, 1902.
*MUNGU AKUBARIKI UNAPOTAFAKARI NENO LAKE*

Leave a Reply