Wivu ni hali ya kuwa na uchungu moyoni pamoja na chuki kutokana na mafanikio ya mtu/watu wengine. wivu ni mbaya na madhara yake ni makubwa pengine zaidi ya ghadhabu na hasira. Hasira ni ukatili na ghadhabu kali ni gharika, lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu?
Wivu unatokana na nini? Kuna mambo mengi yanayosababisha wivu lakini mambo makuu ni…….
1. Matarajiyo yasiyofanikiwa – Mara nyingine unaweza weka matarajio ambayo sio rahisi kufikia, na tunataka yafanyike haraka. Pale ambapo mambo hayaendi kama ulivyotarajia ndipo unakuta unatafuta mtu wa kumlaumu na unapoona mwingine kafanikiwa kwa jambo hilo hilo wivu unaanza kukuingia.
2. Kudhani kuwa unastahili zaidi – Unaweza kudhani kuwa kutokana na elimu yako, kazi yako au hata historia yako basi kuna mambo ambayo unastahili kuwa nayo. Pale ambapo unakuwa hujayapata na kuona watu ambao ulidhani wewe unastahili zaidi yao wamefanikiwa, wivu unaingia maana unaona kama wao hawastahili bali wewe maana uliwadharau.
3. Kutokujiamini – Wivu unaweza kukuingia kama wewe mwenyewe hujiamini, maana kutokana na kutokujiamini hutakuwa tayari kufanya mambo makubwa na utakapoona wengine wanafanya na kufanikiwa utafikiri wanapendelewa na ndipo utakapoanza kuwaonea wivu.
Utajiepusha vipi na wivu?
1. Acha kujilinganisha na wengine na pia usimdharau mwingine. Kila mtu ameumbwa kwa jinsi ya kipekee na tofauti. Mungu anampango na maisha yako na pia na ya mwingine kwa namna tofauti tofauti hivyo usipende kujilinganisha na mwignine au kumdharau mtu yeyote. Hutakiwi kujisikia vibaya pale ambapo unaona kuwa hauna vitu fulani ambavyo wengine wanavyo, Mungu anampango na maisha yako kwa wakati wake.
2. Fikiria na wengine. Umetumia muda mwingi kujifikiria wewe tu na maisha yako ndio maana wivu unapata nafasi, jaribu kufikiria na wengine pia. Angalia ni kwa njia gani unaweza kuwa baraka kwa watu wengine na kwa kufanya hivi utaona furaha na amani ya ndani na kugundua kuwa na wewe pia una kitu cha thamani ndani yako. Wivu hautaweza tena kukupata maana sasa utakuwa ni mtu wa kuwabariki wengine na sio kuwaonea wivu.
3. Kuwa tayari kulipa gharama. Unaweza muoneo wivu mtu sababu ya mafanikio yake kimasomo au kibiashara, je upo tayari kulipia gharama ilikupata mafanikio kama hayo? Hapa sizungumzii fedha bali ile kazi aliyoifanya kufikia hapo alipo, kusoma kwa bidii, kuamka mapema na kufanya kazi kwa bidii, kujitoa n.k. Badala ya kukaa na kuona wivu inuka na wewe ufanye kazi ili upate mafanikio yako.
4. Tumia vipawa vyako. Mungu amekupa vipawa vingi na nafasi nyingi ili kufanikisha maisha yako, badala ya kuangalia wengine wana nini, angalia wewe una nini na tumia ulivyonavyo ili uweze kufanikisha maisha yako na kutimiza ndoto zako. Mungu akubariki sana. Source unknown!