Uamuzi wa Hoyce kuwa na moyo wa aina hiyo ulikuja baada ya kutambua nafasi aliyonayo kwa jamii na kuona wingi wa matatizo waliyonayo Watanzania wenzake na hivyo kufikia uamuzi wa kuanzisha kipindi ambacho kwa sasa kina zaidi ya miaka 5 na bado ameonyesha nia ya dhati kuendeleza kipindi hicho. Kwa kutambua huduma yake kwa jamii, Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga aliwahi kunukuliwa akimtaja Hoyce Temukama mlimbwende bora kuliko wote wakati alipotembelea kituo cha Nunge kilichopo Kigamboni, Dar Es Salaam kinachotumika kutunza wazee wasiojiweza na walemavu wasiokuwa na uwezo. Pamoja ya kujitoa kusaidia Watanzania wenzake walio na uhitaji na kutumia muda wake mwingi katika huduma za kijamii, baadhi ya watu wasio na nia njema na Hoyce wamekuwa wakimwandika vibaya ilimradi tu kumchafulia jina katika jamii inayomzunguka. Mtangazaji wa kipindi cha Mimi na Tanzania, Hoyce Temu akirekodi moja ya kipindi chake cha Mimi na Tanzania na mtoto ambaye aliaga dunia kabla ya matibabu.
Kama Watanzania ambao tunapenda kuona huduma za kijamii zinaboreshwa kupitia kwa Hoyce Temu na kipindi chake cha Mimi na Tanzania tuna wajibu wa kuhakikisha tunaungana kwa pamoja kumsaidia Hoyce kama mwanamke shujaa na mwenye moyo wa huruma kuwasaidia Watanzania ili kufikia malengo ambayo ameweka kuisaidia jamii. Muungano wa Watanzania ndiyo pekee utakaozidi kumfanya Hoyce kuwa na moyo zaidi wa kusaidia Watanzania wenzake wenye uhitaji na amekuwa mtu ambaye anaonekana kuzingatia maoni ambayo anapewa na Watanzania wenye nia njema na yeye ili kuzidi kuwa mtu mwema katika jamii ya Tanzania na dunia kwa ujumla. Hata hivyo licha ya watu wachache kumchafua amekuwa mtu ambaye hajishughulishi kuwajibu wenye nia mbaya na mipango yake kuwasaidia Watanzania na muda mwingi kuendelea kuitumia jamii na kufanya kazi kwenye kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano katika ofisi za Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini. Pia licha ya kazi anazofanya Hoyce kwa sasa anatumia muda wake mwingine kuongeza elimu yake kwa kuchukua PHD ya mambo ya Mawasiliano.