Nataka wewe leo uwe hakimu (Judge), tena si wa mahakama ndogo. Hapa, wewe leo ni jaji wa mahakama ya rufaa. Na unatakiwa kufanya maamuzi juu ya kesi hii na maamuzi yako ni ya mwisho hakuna wakupinga. Nakuletea hawa watu wawili ambao wote wanataka haki itendeke bila kumuonea mtu yoyote kwani “mnyonge mnyongeni haki yake mpeni”! Mtu wa kwanza tutampa jina la Sikudhani. Na mtu wa pili tutampa jina la Sikujua. Sasa Sikudhani na Sikujua wao wenyewe kwa hiyari yao wakaamua kununua shamba pamoja. Wote walitoa kiasi sawa cha fedha kilichohitajika kununua shamba. Wakagawana katika ili kila mtu alime sawa bila ‘kumyonya’ mwenzake. Sikujua hakuwa na pesa za ziada hivyo alitegemea wangesaidiana na rafiki yake ili waweze kutafuta pesa pamoja kwa kuuza mazao watakayo lima. Sasa katika harakati za kuanza kuandaa shamba ili wapande mazao ilikuwa kama ifuatavyo -:
SIKUDHANI: Sikudhani yeye hakudhania kuwa lile shamba lina ubora na virutubisho vyoyote ambavyo vingewezesha kuzaa matunda au mazao. Hakuona kama kuna umuhimu wa kutumia nguvu na pesa zake kuwekeza kwenye hilo shamba kwani halina thamani hiyo. Hakudhania kuwa kuchukua pesa zake na kutafuta watu wa kulimaa na kuongeza mbole kwenye hilo shamba ni wazo la busara. Hivyo aliachana na hilo shamba bila kujali chochote. Hata pale Sikujua alipo msihi kuwa jaribu hata mara moja kabla ya kusema haifai, lakini Sikudhani alikataa kata kata tena kwa dharau na dhihaka nyingi; “shamba lenyewe lipo sehemu kavu. Hakuna hata maji pamekauka kama jangwani nitapata nini hapo! Angalia lipo kwenye muinuko mvua ikija mazao yote yatachukuliwa na mvua. Sina shida nao, hela ya kununua vyakula ninayo mpaka siku nakufa.”!
SIKUJUA: Yeye alikuwa na imani kuwa anaweza kupata kitu katika shamba lile japo hakujua ni kwa kiasi gani. Alijua kuwa linadhamani yakutosha kuwekeza nguvu zake hapo kwani ametumia pesa yake kulinunua. Sikujua yeye alikuwa mtu mwenye hali duni hivyo shamba ndiyo ilikuwa tuamini lake!
Basi, Sikujua alianza kuandaa shamba kwa jembe lake dogo la mkono. Kila siku anaamka hasubuhi na mapema, anaandaa chakula na maji ya kunywa anaenda shambani kuanzia saa kumi na moja (5am) asubuhi mpaka saa kumi na moja (5pm) jioni. Akatoa magugu yote, upande wake na upande wa Sikudhani. Kwasababu alikuwa hana pesa, hivyo akamwambia Sikudhani kuwa; nimetoa magugu na nyasi zote shambani naomba unisaidie hela kidogo ya kununua mbegu ili nipande mazao. Nitapanda hata upande wako. Kwa kuzuiya mmonyoko ningependa kuanza kwa kupanda miti ya maembe pembezoni mwa shamba kwanza. Sikudhani akamjibu kwa dhiaka; “nipishe huko wewe mjinga, sina pesa za kupoteza mimi.”! Sikujua kwa upole na unyonge mwingi akaondoka huku akisema “asante Sikudhani.” Sikujua akatafuta pesa za kununua mbegu kutoka kwa mama yake mzazi akampatia. Japo mama yake alikuwa na shida nyingi lakini hakuweza kumtupa mwanae kwani naye kama ilivyo kuwa kwa Sikujua aliamini kuwa mwanaye atapata kitu kwenye lile shamba na hato hitajika kumsaidia tena. Sikujua alimshukuru sana mama yake si tu kwa msaada wa pesa aliyompatia bali kwa kumsaidia kujihifadhi pamoja na wanawe kwenye kibanda alichokuwa anaishi.
Sikujua akapanda mbegu 20 za mti wa maembe kuzunguka eneo lake tu. Hakupanda hata mbegu moja kwenye eneo la Sikudhani! Kwasababu pale ni pakavu sana basi ilimbidi aende mbali kuchota maji ya kumwagilia ili mbegu zake zisikauke. Sikujua alitembea peku peku kwani alikuwa hana uwezo wa kununua viatu. Pesa alizokuanazo kidogo alinunua mbolea akamwagia kwenye mbegu. Mvua ikaanza kunyesha.
Kwakuwa mvua ilikuwa inanyesha kubwa akahofia mbegu zake kuchukuliwa na maji kwani pale kulikuwa na mteremko. Basi akaamua kwenda kusomba mawe ili aweke pembezoni mwa shamba kuzuiya madhara ya mvua kwa mbegu zake. wakati anarudi kutoka kutafuta mawe akiwa njiani mvua ikaanza kunyesha. Pale hapakuwa na sehemu ya kujihifadhi hivyo ilimbidi aendelee na safari. Aliloana sana.
Akafika shambani na kuweka mawe huku mvua ikiendelea kunyesha lakini hakuacha kwani mbegu zile zilikuwa muhimu sana kwake kuliko kuloana na mvua haswa akikumbuka kuwa pesa alizo nunulia mbegu amepewa na mama yake mzazi ambaye ni mzee na masikini kama yeye! Mvua ilikuwa ni kubwa sana, mbegu 19 kati ya ishirini zilisombwa na maji. Ikabakia moja tu ambayo ilikuwa katikati ambapo ndipo panagawa mpaka wa eneo lake na eneo la Sikudhani. Sikujua hakukata tamaa. Akalinda mbegu hiyo moja. Mti ukawa mkubwa. Sikudhani alipo ona mti unakuwa mkubwa kama ilivyo kawaida yake na dharau nyingi. Akawa anasema “huo wala hauto toa maembe. Huo mti ni tasa hauzai unajisumbua tu!”
Baada ya muda kidogo, mti ule ukaanza kuota maembe. Ukatoa maembe makubwa sana tena maembe “dodo”! Maembe yalikuwa mengi sana na matawi yalikuwa marefu hivyo yalipo anguka chini mengine yaliangukia upande wa Sikudhani! Sikujua akayakusanya maembe akapeleka sokoni akauza akapata pesa za kujikimu. Mti unaendelea kutoa maembe na Sikujua anafurahia faida anayo pata kutokanana jasho lake. Ameweza kununua ng’ombe anapata mbolea na kuuza maziwa pia anatumia ng’ombe kulimia. Sikujua sasa amejenga na nyumba anaishi na wanawe! Bahati mbaya mama yake mzazi Sikujua aliugua na kufariki kabla ya mti kuanza kutoa matunda. Alibahatika kuuona ulivyo kuwa mkubwa lakini hakuona matunda yalivyo toka. Hii inamsikitisha sana Sikujua na baadhi ya ndugu zake kwani wanatamani sana mama yao angeona na kuonja matunda angalau kidogo. Mungu si Athumani, Sikujua amebahatika kupata wajukuu. Nao wanapenda sana maembe. Wanafurahiya kunywa maji ya maembe kila siku! Chakushangaza, Sikudhani sasa naye ananyemelea maembe ya Sikujua! Anasema yale yanayo angukia upande wake ni yakwake! Sikujua hataki hata kusikia habari hiyo! Sasa hivi Sikudhani anaumwa anahitaji hela za matibabu matokeo yake anataka achukuwe maembe aende kuuza ili apate pesa za matibabu. Lakini Sikujua hataki kusikia habari hiyo kwani bado anakumbuka matusi, dharau, na dhihaka alizo mfanyia! Siku moja, Sikudhani akamwambia Sikujua kwa sauti ya ukali kuwa; hata kama hilo shamba tuligawana katikati kwaajili ya kulima, lakini hati miliki ya shamba inaonyesha wote wawili ni wamiliki wa hilo shamba. Hivyo nayeye anastahili kupata maembe yaliyopo shambani hapo! Sikujua amekataa na sasa amekimbilia mahakamani kupata haki yake!Ni nani haswa anastahili kula matunda kati ya Sikudhani na Sikujua? Na kuna ubaya wowote Sikujua kumkatalia Sikudhani kuchukua maembe? Tafakari kwa kina toa hukumu ya haki na sahii!
Tafadhali: picha zilizo tumika hazina huusiano wa moja kwa moja na hadithi hii.