“UPINZANI TANZANIA UMEPOOZA, BADILISHENI MBINU ZA MAPAMBANO. MSIPO BADILIKA MTAZAA UASI WA NCHI.”-Peter Sarungi

fb_img_1477317177774Nchi yoyote inayofuata utawala na siasa za kidemokrasia ni lazima kuwe na upinzani imara kwa manufaa ya utawala bora kwa nchi. Tanzania ni moja ya nchi yenye siasa za kidemokrasia kupitia vyama vingi. Moja ya Upinzani Imara kuwahi kutokea Tanzania ni pale vyama vinne vya siasa vilivyoamua kujiunga pamoja na kuunda muungano uitwao UKAWA. Ni Ukweli kuwa nguvu kubwa ya UKAWA inatokana na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na hii imetokana na mbinu nyingi za siasa zilizotumiwa na CHADEMA kwa kipindi cha miaka 10 ya utawala wa Mh. J. Kikwete ambayo iliweza kuimarisha Upinzani nchini. Tulishuhudia mbinu mbalimbali zilizo teka fikra za watanzania pamoja na vyombo vya habari Mfano Operation Sangara iliyofanyika kanda ya ziwa iliyovuna wafuasi kwa wingi kama Sangara anavyovuliwa baharini, Kulikuwepo na vuguvugu la kutaka mabadiliko M4C iliyorindima kwa wananchi kupitia makundi mbalimbali ya vijana, wanavyuo, wafanyakazi, wanawake na kada mabalimbali na matokeo yake tulishuhudia migomo na maandamano ya kudai haki na kutaka kusikilizwa kutoka kwa makundi hayo kama vile migomo ya waalimu nchi nzima, migomo ya wanavyuo, migomo ya wananchi kama kule Mtwara na migomo ya wafanyakazi nchi nzima. Tulishuhudia Sera na kelele za kupambana na Rushwa ziliyoibua madudu mengi yaliyokuwa yakifanywa na watawala pamoja na watumishi wa Umma kama vile Scandal za Richmond, EPA, Meremeta, Tegeta Escrow, IPL, Kagoda na nyingi zilizo ibuliwa na kuiacha Serikali na Chama tawala ikiwa uchi kisiasa na hapo ndipo neno FISADI na Ufisadi lilipopata umaarufu. pamoja na hayo Upinzania uliweza kubadili fikra ya wananchi juu ya rasilimali zao, kufuatilia mapato na matumizi ya Serikali pamoja na kujua Haki za binadamu na haki za kikatiba kama vile Uhuru wa kujieleza, kutoa maoni yako na kusikilizwa. Kwa jitihada hizi za Upinzani Imara tuliweza kuona Serikali ikitoa maelezo ya kujitetea, ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni njia ya kurespond malalamiko ya wananchi. Yote haya yalifanyika kwa sababu ya Upinzani Imara.

Leo tupo katika utawala wa tano, utawala unaojinasibu kwa maneno ya HAPA KAZI TU, Utawala uliojiapiza kutetea wanachi wanyonge walio wengi na walio teseka kwa mda mrefu, Utawala uliojiapiza kupambana na Mafisadi, Utawala uliojiapiza kurudisha nidhamu ya watumishi wa umma juu ya rasilimali za nchi, Utawala usio hitaji siasa wakati wa kazi, Utawala usio taka kugaramia garama za demokrasia kama kuonesha Bunge Live, Utawala unaochukua maamuzi kwa maslahi ya nchi, Utawala uliojiapiza kupita katika njia za ahadi za Raisi na kuzitimiza kama vile kufufua shirika la ndege ATC, Utawala usio hitaji kupelekeshwa wala kujaribiwa, Utawala ulio amua kwenda kinyume na utawala uliopita wa JK yaani utawala ulio amua kufanya mengi yaliyo lalamikiwa na wapinzani wa JK na kutofanya yale mema yaliyofurahiwa na wapinzani wa JK kama vile kulinda na kuheshimu demokrasia.

Kwa zama hizi za JPM, Upinzani unaonekana kupooza sana nchini. Kupooza kwa Upinzani kunatokana na matokeo hasi ya mikakati yao ya kisiasa wanayofanya dhidi ya mikakati ya kisiasa inayofanywa na serikali ya JPM kwa wapinzani. Mikakati inayofanywa na serikali ya JPM ni ya makusudi na yenye ufundi wa hali ya juu na yenye kufuata udhaifu wa sheria zetu zinazotungwa bungeni. JPM amesoma tabia na desturi za wapinzani, amesoma njia zao na mbinu zao, amesoma uwezo wa watu muhimu katika upinzani (key people) na mwisho akasoma udhaifu uliopo katika kila idara ya uendeshaji wa Upinzani. Matokeo yake ni JPM kuja na mbinu tofauti na zile zilizo zoeleka na Upinzani kipindi cha JK, ndio maana ameweza kudhibiti vyanzo vyote vya kuimarisha Upinzani kama vile Bunge, Siasa za majukwaa, Maandamano, Migomo, vyanzo vya mapato, demokrasia katika chaguzi za sasa na mengine mengi yanayoweza kififisha demokrasia na vyama vya Upinzani.

Kwa Bahati mbaya sana, Upinzani bado haujashitukia mchezo unavyochezwa, bado wana mikakati, njia, tabia, desturi na mbinu zilezile na key people walewale waliodumu kwa miaka 10 ya JK. Bado wapinzani hawajabadilika kwa fikra na mienendo, Mfano: Bado wanaamini katika maandamano na migomo, Bado wanaamini katika matamko yasiyo fanyiwa kazi na bado wanaamini katika kususia vikao hata vile muhimu kisa tu wanatendewa ndivyo sivyo. Kwa muundo huu wa Upinzani usiobadilika na kwa mikakati hii JPM kuna uwezekano Upinzani ukafifia na kudorora ifikapo 2020, kuna haja ya Upinzani kubadilika tena haraka ili kutopoteza imani waliyoijenga kwa muda mrefu kwa wananchi.

Kuna hasara kubwa kama upinzani hautabadilika kutoka sasa. Tabia ya kususa vikao mbalimbali halali vya kuwasemea wananchi walio wachagua hauna tija kwa sasa maana una nyima haki ya wananchi kuwakilishwa na mwisho wa siku yanapatikana maamuzi yasiyojali wananchi walio wengi,
mfano: upinzani ulisusia Bunge la katiba na matokeo yake ikapatikana katiba yenye maslahi ya chama kimoja, Wamesusia Bunge la bajeti na matokeo yake ikapatikana bajeti iliyokuwa na mapungufu mengi ya sera za uchumi, wamesusia uchaguzi wa meya wa kinondoni na matokeo yake amepatikana meya kwa kura 18 za ccm. Hii tabia inakera sana na inawagarimu wananchi walio wapigia kura katika mazingira magumu na wengine walipata ulemavu wa kudumu katika kutimiza na kulinda haki zao. Kwanini msipambane kwa njia zote katika kupata haki zenu? kwanini mkimbilie kususa na kutoka nje? kwa nini mnafanya siasa ya maneno badala ya kufanya siasa ya matendo?
Mmeitisha maandamano ya nchi nzima, mmekuja na UKUTA na mwisho mka airisha kwa sababu ya uimara wa JPM.

Na Peter Sarungi (Next Speaker, Baba Pilato)
Na Peter Sarungi (Next Speaker, Baba Pilato)

#Mytake
Upinzani ukiendelea kufanya siasa za maneno na kuacha matendo nyuma, Upinzani ukiendelea kung’ang’ania mbinu na mikakati ya kipindi cha JK bila kubadilika, watajikuta wanapandikiza mbegu za chuki, hasira, vurugu na uhasama dhidi ya Serikali na itafika kipindi watazaa WAASI wa nchi watao sababisha Machafuko ya nchi. Upinzani hauna chaguo mbadala zaidi ya kubadili mbinu na miakakati ya siasa zao maana ni kweli bado tunahitaji uimara wa upinzani nchini katika kuleta mabadiliko na maendeleo ya wananchi. Siasa zina Ishi na zitaendelwa kuwepo hata aje malaika kutoka mbinguni kuja kutawala bado siasa itazaa wapinzani kwa hoja na kwa kupingana katika fikra na ndio maana hata katika utawala wa mbinguni bado siasa ilijitokeza na malaika mkuu akahasi na akawa mpinzani mkuu wa Mungu. pamoja na hayo bado Mungu alimpa Shetani Uhuru wa kufanya siasa ili apate wafuasi ingawa Mungu alikuwa na sababu na uwezo wote wa kuangamiza upinzani wa Shetani kwa watu wake.

asanteni.

Leave a Reply