Wakati fulani naonaga hakuna haja ya kuangaika kusoma mpaka hata PHD na Uprofesa ikiwa haisaidii kutatua matatizo ya jamii hasa ukizingatia jamii inakuchukulia kama kioo cha kujifunza. Aibu hizi za wasomi kutumia akili za kushikishwa zinazowakumba wengi hasa wasomi wa kiwango cha juu sio Tanzania tu bali ni karibia Afrika nzima, madudu haya yanasababishwa na uwepo wa mifumo kandamizi na mibovu ya uendeshaji wa siasa ndani na nje ya vyama vya siasa. Katika nchi za Afrika, Mwanasiasa ndiye mtu anaye ogopeka zaidi, kuheshimika zaidi, kuthaminiwa zaidi, mwenye nguvu ya kuishi maisha ya Mungu Mtu, siasa ndiyo kazi iliyo karibu sana na fursa mbalimbali za uchumi hivyo katika nchi zetu basi ni wengi wanao tamani kufanya siasa ili tu waishi maisha mazuri.
Kutokana na mfumo wa vyama vingi nchini, ina mlazimu kila mwenye ndoto ya kuwa kiongozi basi apitie kwenye chama cha siasa ili aweze kufanya siasa. Unapo amua kuchagua chama ni lazima uangalie kile chama kitakacho saidia kufikia malengo yako yawe ya karibu ama ya mbali. Kwa Tanzania yetu, unaweza kujiunga na chama tawala, umoja wa Ukawa ama ACT na vyama vingine vingi vinavyofika 25+. Watu wazima wengi na wazee wengi hupendelea kujiunga na chama tawala kwa lengo lakufanya siasa ya malengo ya karibu maana wana amini kwa umri waliofikia hawana ndoto za miaka mingi mbele, Lakini pia hawana nguvu na hari ya kufanya harakati na siaaa za vuguvugu. Vijana wengi wanapendelea kujiunga na vyama vya upinzani kwa sababu ya ndoto walizonazo, nguvu pamoja na utayari wa kufanya siasa za vuguvugu na harakati, lakini pia wanakuwa wapo katika umri wa kutafuta maisha mazuri hivyo wapo tayari kuthubutu na kujaribu mambo mbalimbali katika utafutaji wao. Na kinyume cha hapo basi kijana anayejiunga na chama tawala huwa na fikra kwamba chama tawala kitashikilia dola kwa miaka mingi itakayoweza ku cover miaka aliyo nayo hadi uzeeni…??? , vivyo hivyo kwa mtu mzima ama mzee kujiunga na upinzani huwa na imani kwamba chama tawala hakina miaka mingi katika kushikilia dola ama ana amini kuwa uchaguzi ujao ndio chama chake cha upinzani kitachukua dola…???
Hivyo unapojiunga na vyama hivyo utasajiliwa na kupewa katiba kama muongozo wa taratibu zote za chama husika, ndani ya katiba utakuta kuna itikadi, taratibu za wewe kufanya siasa na kuwa kiongozi, taratibu za kukuadhibu, haki na wajibu wako pamoja na maelezo mengi yanayokueleza kipi cha kufanya na kipi usifanye. Katiba hizi zinakuwa zinatengenezwa kwaajili ya kulinda maslahi mapana ya chama ya muda wote bila kujali maslahi ya Taifa na ya mwanachama husika, na hichi ndicho chanzo za wasomi wetu kuwa watumwa na vikra na matendo, yaani na usomi wao wote wanajikuta maarifa yao yamebanwa kwenye katiba za vyama. Mtaka cha Uvunguni Sharti Akunje goti na kuinama..???. Ukitaka kula tamu ya siasa na uongozi basi sharti uiname kwenye fikra zetu hata kama ni mbovu, ovu, duni, zenye uongo, propaganda, fitna, unafiki, ghiliba, chuki, uhasama, kinyongo, vurugu, umbea, ushirikina, uuaji, mateso, rushwa, udini, ukabila, ukanda na mambo mengi sharti ukubaliane nayo na uwe tayari kuyatetea na kujitoa muhanga maana chama siku zote huwa akikosei. Daaaah, inapofika hapa ndipo akili za kisomi zinawekwa pembeni na kuvikwa sharti la kupiga magoti na kuinama maana anaaminishwa kuwa hizo ndizo mbinu za ushindi katika siasa. Huu mfumo umedumaza akili na fikra za wafuasi na wana siasa wa vyama husika kiasi kwamba wapo tayari kubadili nyekundu kuwa nyeusi kwa njia zozote na kuhalalisha, wapo tayari kudhalilisha utu na elimu yao kwa maslahi yake na ya chama chake, wapo tayari kupinga kila kitu kinachofanywa na mpinzani wake hata kama ni kizuri na jema na wapo tayari kukubali kila kitu kinachosemwa na chama chake hata kama ni baya na ovu. Hizi ndizo akili ninazozipinga maana hazina maslahi ya kweli na mapana ya Taifa, wapo tayari taifa liangamie ili walinde maslahi yao na wapo tayari kuchafua hali ya hewa kwa maslahi yao. Alafu wanajiita majina ya kondoo kama Wazalendo, Wakombozi na Wanaharakati wakati ni mbwa mwitu wasio kuwa na maslahi na Taifa na watu wake.
Kila mtu amepewa akili na utashi wa kuamua jambo na kutumia fikra na maono yake, hivyo kuwa tofauti au kuwa pekee ni jambo linalojitokeza mara nyingi,ila tatizo ni nani mwenye uwezo wa kusimamia na kueleza fikra zake zilizo tofauti na mifumo ya vyama vyetu? ni nani anayeweza kukosoa na kupinga maamuzi na mambo mengine yaliyopo kwenye vyama vyetu? ni nani anayeweza kumkosoa Mkuu wa kaya katika chama tawala na akaendelea kuwa mwanachama? ni nani anayeweza kumkosoa Mtu huru katika chama chake na akawndelea kuwa mwanachama? Ukiweza kufanya tofauti na mifumo ilivyo basi jiandae kutapikwa na mifumo husika, Ndio maana tunaimba CCM ni ile ile na CDM ni ile ile. Prof. Lipumba pamoja na kukimbia vita vya mwaka jana lakini bado ana wafuasi waliopenda stayle yake ya kukimbia, JPM pamoja na kuapa kutoshirikisha mpinzani katika serikali yake lakini ameweza kumchagua Agustino Mrema katika serikali yake.
Kuna watu walio jaribu kuvunja tabia za kutumia akili za mfumo badala ya kutumia zake, walikataa kukubali kila kitu cha chama chake ama kukataa kila kitu cha mpinzani wake, waliamua kupaza sauti zao kuu zilizotoa fikra kinzani na chama chake. Pamoja na mfumo kuwatema na wakaitwa majina ya kudhiaki, majina ya matusi, wakazushiwa kashfa nyingi, wakalaaniwa kwa maneno, wakaombewa na kutabiriwa vifo, lakini waliweza kusimama na kusema kwa kutumia akili zao. Watu hao ni pamoja na Mh. Edward Lowassa, MSaid Arfito Zuberi, Said Arfi, Marehemu Deo Filikunjombe, Mh. Raila Odinga, Mh. Ababu namwamba, Mh. Kiiza Besige, Mh. Donald Trump na wengine walio itwa WASALITI kwa kusema fikra zao zilizo tofauti na mifumo ya vyama vyao. Wengi wetu tunaendelea kuwa wafuasi, wananchama na wakereketwa wa vyama bila hata kushirikisha akili zetu na mwisho wa siku tunakubali kila kitu kinachosemwa na kamati kuu isiyozidi hata watu 50 wanaotuamulia sisi tulio zaidi ya milioni kadhaaa.. (80/20 rule) kisha tunafuata maamuzi hayo kwa nguvu zote hata kama ni mabovu. Na tunapinga kila jambo lilifanywa na mpinzani wako hata kama ni la maendeleo na hapo ndipo unapoweka pembeni maslahi ya Taifa hili.#Mytake
1. Tuanhitaji vyama vya siasa visizo na kikwazo katika fikra, vyama vyenye kuruhusu fikra mbadala, fikra huru zisikilizwe, vyama vyenye kuwa na ajenda yenye masalhi makubwa kwa taifa, vyama vyenye kutengeneza wafuasi, wanachama na wakereketwa huru wenye kuhoji maamuzi ya kamati kuu.
2. Tunahitaji wanachama wasomi wanao tumia akili na elimu zao katika kufanya siasa, wanaojali maslahi ya taifa.
3. Tunahitaji upekee, maana upekee unaleta utofauti, utofauti unaleta mabadiliko na mabadiliko huleta Maendeleo