WARAKA WANGU KWA UPINZANI NA SERIKALI- Mkandara Ebbie

Kwa heshima na taadhima natanguliza TAIFA KWANZA kama msingi wa waraka huu kuyazungumzia yalotusibu sisi wananchi kutokana na mtafaruku wa ajabu kabisa usiozingatia Maadili ya utumishi katika mihimili ya nchi yetu.Ni aibu kubwa kwa taifa letu maana imekuwa kama maonyesho ya sinema.

Ndugu zangu wa Upinzani, binafsi mimi sielewi kabisa kilichowasibu hata mkafikia kuchukua hatua ya kutowawakillisha wananchi wenu mkachagua kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge wakati wa vikao vya bunge ilihali hii ndio kazi mlotumwa na wananchi kuifanya. Mmechagua yenu dhidi ya wananchi – Sielewi kabisa usema kweli…

Hoja yenu kubwa nilowahi kuisikia kuwa hii ni moja ya jitihada zenu za kupigania Demokrasia ambayo kwa tafsiri yenu imeporwa na Serikali ya Magufuli. Demokrasia ipi? Kule kufukuzwa kwa baadhi ya Wabunge walovunja kanuni za Bunge wakahukumiwa na kamati ya Bunge, hivyo kuihsia kutokuwa na imani na Naibu Spika!

Kama sababu ni hii jiulizeni wenyewe nini sheria ya kufikisha madai haya na utaratibu gani unatakiwa kufanyika kulingana na kanuni za Bunge. Bila shaka kama tunazungumzia Demokrasia yenyewe Ushindi wenu utapatikana tu ikiwa Upinzani wataweza kushinda kwa kura zaidi kutokuwa na Imani na Naibu Spika. Nje ya hapo ni Demokrasia gani mnayotaka itumike! Rais atumbue Jipu kama mlivyotaka aingilie uchaguzi wa Zanzibar! Na hii ndio Demokrasia mnayolilia?

Nakumbuka vizuri sana, awamu ilopita, Kiongozi Zitto Kabwe Ruyagwa aliwahi kufanya utaratibu wa kukusanya saini za Wabunge kwa kutokuwa na Imani na Waziri mkuu wakati huo akiwa Mh. Mizengo Pinda. Sikuona mkitoka nje kwa sababu Waziri mkuu aliendelea kuwa katika nafasi yake..

Nakumbuka pia wakati Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete alipokuja Bungeni kuhutubia kwa mara ya kwanza 2010, mlitoka nje kwa kutomtambua, pia kuingia kwa John Magufuli mlifanya hivyo hivyo kwa kutomtambua rais wa Zanzibar Mohammed Shein lakini maajabu ya Mussa wakati wote mkakubali kuapishwa kama wabunge wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya viongozi hao hao…

Sasa najiuliza kwa nini mliendelea kuwepo Bungeni? Leo mnaweka madai ya kufungwa midomo kwa kupigania kipi haswa ambacho sisi wananchi tumeshindwa kukielewa! na pengine nirudi tena katika swala la Television na #BungeLIve.

Kama kweli hii ndio sababu, mbona mnaingilia kazi isokuwa yenu? Ni wananchi walokosa onyesho hili wanaotakiwa kuweka madai yao aidha kwa kuonyesha umuhimu wa swala hili kwao wao. wanaweza andamana hadi Ofisi ya Waziri wa sanaa na Michezo Nape Nnauye bila kushinikizwa na viongozi wa vyama bali kwa utashi wao wenyewe na kueleza malalamiko yao wakiwa na sababu dhidi ya zile zilizoainishwa na serikali.

Wanaodai #BungeLive ni Wananchi sio nyie Wabunge na wala sio kazi mlotumwa na wananchi na kama ndivyo onyesheni ushahidi bungeni au mahakamani. Mwanamuziki huwezi kugoma Kuimba ukumbini ati kwa sababu Clouds wamekataa kurusha video ya muziki wako LIVE ukadai kuwa haya ni matakwa ya wananchi!,Acha wao waweke madai maana wao ndio wanaolipa fedha toka kodi zao.

Serikali ya kiongozi John Magufuli, nawaomba, tena nawaomba sana maadam mihimili yote mitatu ipo chini ya JMT. Hakikisha hawa Wabunge wanarudi Bungeni na kufanya kazi walokabidhiwa na wananchi, laa sivyo wasipokee mishahara na posho zao pasipo kufanya. KAZI walopewa sio kwenda kujaza form za malipo kisha watimke bali ni kuwakilisha wananchi wa majimbo yao Bungeni. Na ikishindikana kabisa basi baada ya vikao hivi tumia Nguvu ya Dola na kuvunja Bunge hili ili Uchaguzi mpya Ufanyike tuone kama watarudi Bungeni tena maana wananchi hatuwezi kuvumilia Uhuni unaofanyika.

Na litakuwa fundisho na mwisho wa wananchi kuchagua viongozi wababaishaji wanaoweka maslahi yao na vyama vyao mbele ya maslahi ya Taifa kwanza, Nidhamu na Maadili ni nguzo pekee ya Utawala bora. Na Bunge ni sehemu muhimu ya Utawala wasifikirie wao wako nje ya Utawala maana wanatakiwa kushiriki katika maamuzi na katika nafasi zao. Tukiyapuuza ama kuyakana haya kwa kuoneana Huruma na Aibu kwa sababu za kujuana itafika wakati hawa watu wataingia na Mbwa Msikitini!

Aslaam Aleikum – Ramadhan Kareem

Leave a Reply