Nakumbuka nimeanza kutambua haki yangu ya kupiga kura mwaka 2000 nilipokuwa kidato cha kwanza na nilishiriki nikiwa na uwezo wa kupambanua sera, ahadi na siasa za wagombea. Hivyo nilishiriki mwaka 2000, 2005, 2010 na 2015. Takribani awamu tatu za utawala nazishuhudia mpaka sasa.
Wanasiasa wengi waligeuza siasa kuwa ni uwanja wa kushawishi kwa kusema uongo wakati wakiomba kura, kuna wakati ilijengeka kuwa ili upate uongozi basi ni lazima uwe na pesa au uwe na uwezo wa kuunda uongo na kuupamba ukiwa unaomba kura.
Uchaguzi ulioisha 2015 umeshitua fikra zangu na kasumba niliyokuwa nayo ya muda mrefu ya kuamini kuwa siasa ni uhodari wa kusema uongo. Upepo ulikuwa ukibadilika kila wakati hadi ikafika sehemu wanasiasa wakakubali ukweli utawale katika hoja zao na ahadi zao.
Nimekuwa nikimsikiliza na kufuatilia kauli za Mh. JPM tangu alivyokuwa akijinadi na kuomba kura hadi alipoanza kazi ya uraisi na nimegundua kuwa Mwisho wa Uongozi na Utendaji wa Mazoea umefika. Nampongeza sana Mh. JPM kwa kuongoza kwa kufuata kauli zake toka alipokuwa akijinadi. Maana dhamira yake na kauli zake hazijabadilika tangu alivyoomba kura hadi sasa.
Hii inaashiria nini? Inashiria kuwa huko tuendako kuna majipu ya mazoea yatatumbuliwa sana. Ni vizuri watanzania tukaanza kuelewa maona ya Raisi hasa kwa kubadilika katika uongozi na utendaji unapokuwa unapewa dhamana au kazi katika idara za serikali. Kufanya kazi kwa mazoea pasipo kujali maslahi ya Taifa na wanyonge, kufanya kazi pasipo kufuata taratibu na sheria za nchi, kufanya kazi kwa kutumia cheo vibaya ni hatari kwa zama hizi za JPM.
Ni vizuri tukajitathmini je, mazoea tuliyonayo yanafaa kwa zama hizi za HAPA KAZI TU? Kama hazifai basi badili gear angani na ucheze ngoma iliyopo.
Na Peter Sarungi