Watu wenye ulemavu ni moja ya jamii iliyo katika makundi nyonge (kwa sasa tumefika milioni 4 kwa idadi). Makundi mengine ni kama wazee, watoto na wanawake, makundi haya yanaitwa ni makundi nyonge kwa sababu yana mahitaji maalumu ya kibinadamu na hayawezi kumudu ushindani ulio sawa katika jamii hivyo ni lazima jamii pamoja na serikali iyatizame kwa jicho la tatu lenye utu, huruma na upendo ili nao wajione wapo katika nchi yao na waweze kuonesha uwezo wao ambao Mungu amewakirimu pasipo kujali mapungufu waliyo nayo.
Mimi ni Mlemavu lakini hata wewe ni Mlemavu mtarajiwa maana kama bado unaishi duniani basi jua Mungu bado anaendeleza uumbaji wake kwako. Hivyo linapotokea jambo linalohusu ulemavu basi jihisi na wewe ni mhusika kwa namna moja ama nyingine.
Katika uchaguzi uliopita 2015, nilitoa tamko kupitia jumuiya za watu wenye ulemavu Tanzania ambao ulilenga kueleza changamoto za walemavu pamoja na mapendekezo yake. Changamto kuu nilizoziainisha kwa msisitizo ni ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika vyombo vya maamuzi pamoja na muundo wa kusimamia maswala ya watu wenye ulemavu. Niliamini kuwa ili kutibu changamoto hizi za elimu, ajira, afya, uchumi, siasa na huduma zingine ni vizuri tukashirikishwa katika kupika chakula na kukiandaa mezani.
Nilifarijika sana baada ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza baraza la Mawaziri pamoja na muundo wa wizara zake, kwa kweli mhe. JPM alitutendea haki ambayo haikuwahi kutendwa na tawala tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi. JPM alisikia kilio cha watu wenye ulemavu kwa kutenga wizara itakayo husika na maswala ya walemavu tena ikiwa chini ya ofisi ya waziri mkuu kama tulivyotoa kwenye tamko na pia akateua waziri mwenye asili ya ulemavu (dr. Abdallah posy) na makatibu wa wizara wawili wenye ulemavu akiwemo mwanasiasa Amon Mpanju ili kushiriki kupika chakula cha walemavu. Hakika baada ya uteuzi huu, jamii ya qatu wenye walemavu tulianza kuona nuru na kuona matumaini ya kula chakula tulichoshiriki kukipika na kukiandaa mezani. Nampongeza sana Raisi kwa moyo huu wa kujali makundi manyonge katika jamii(Mungu azidi kumpa afya tele na azidi kutetea wanyonge kama anavyofanya sasa)
TATIZO NI NINI?????
Kwa mtazamo wangu, bado naona hakuna mabadiliko chanya yanayoletwa na wizara hii hasa kutoka kwa waziri husika Mh.Posy. Bado mifumo ya unyonyaji imeendelea kuwepo kwenye vyama vya watu wenye ulemavu, bado uchumi umezidi kudorora kwa watu wenye ulemavu, bado Elimu imekua duni na garama kwa watu wenye ulemavu, Bado siasa haiwatambui watu wenye ulemavu kwa vitendo, Bado sheria No 10 ya watu wenye ulemavu imewekwa kando, Bado ajiri imekuwa ngumu na ya kubagua watu wenye ulemavu na bado huduma bora imekuwa ni kitendawili kwa watu wenye ulemavu.
Je ni nani wa kututetea? Ni nani wa kutusemea kama sio Mh. Posy na wenzake akina stella ikupa, Dr. Macha, amina mollel, amon mpanju na wengine walio katika kundi hili?. Ni nani wa kulaumiwa ikiwa JPM ametupa nafasi kupitia hawa wenzetu alafu wamekaa kimya? Ni nani wa kuonesha mfano na kuaminisha jamii juu ya uwezo wetu kama sio akina Posy, Mpanju, macha, stella na wenzake? Ni nani wa kupiga kelele juu ya mateso na manyanyaso wanayoyapata wafanyabiashara walemavu wa Tanzania kama sio akina Mh. Posy, Mpanju na wenzake waliopata fursa? Ni nani wa kutuunganisha watu wenye ulemavu na kupata fursa za uchumi na siasa kama sio hawa walio teuliwa na JPM? Mbona wamejisahau utafikiri hawajatoka katika kundi hili? Au wanadhani fursa waliyopata ni kwaajili yao peke yao? Au ndo kusema ni aibu na dhihaka kuwa mlemavu na kutetea jamiiyako? Mbona kasi ya JPM inawaacha mbali? Tatizo ni nini?Tulikaa kimya na kuwapa ushirikiano ili kuona matunda ya kushirikishwa katika kupika chakula lakini inakaribia mwaka sasa hatuoni kama chakula mnachotupikia ni kizuri…
Tafakarini na chukueni Hatua….